Ticker

6/recent/ticker-posts

Sababu za vigogo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Kufyekwa zatajwaDar es Salaam. Baada ya kiti cha ukurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuwa cha moto kwa kila anayeingia, wadau wa sekta hiyo wamependekeza kuboreshwa na kusimamiwa mifumo ili kuwa muarobaini wa changamoto zinazowang’oa kila uchwao.

Hoja hizo za wadau zinaibuka wakati juzi, Rais Samia Suluhu Hassan, akimtengua mkurugenzi mkuu wa TPA, Erick Hamissi na kuingia kwenye orodha ya bosi wa sita kung’olewa kwa kipindi cha miaka 10.

Wadau hao walisema upotevu wa mapato, urasimu na ucheleweshwaji wa huduma si kosa la mtu mmoja, bali ni matokeo ya changamoto za mifumo ya kielektroniki, inayofanya mamlaka hiyo ishindwe kuendeshwa kwa tija.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Usafirishaji Mizigo Bandarini ya Epic Cargo Ltd, Mhandisi Tony Swai alisema jana kuwa ni vyema watu kuepuka kuingilia mifumo (teknolojia) ya shughuli za bandari, “tukienda Mlimani City unahudumiwa na mfumo, uwanja wa ndege vivyo hivyo, kwa nini tunashindwa kufanya hivi bandarini? Kinashindikana nini kutumia mfumo kutoa gari bandarini.”


Mhandisi Swai ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la Ujuzi na Usafirishaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), alisema tija ndogo inayoshuhudiwa katika bandari inatokana na binadamu kuingilia shughuli zilizopaswa kufanywa na mifumo.

“Utawaonea watu bure, utamuondoa kila mtu, lakini shida ipo kwenye mifumo ndiyo inayokwamisha. Kinachotakiwa kufanywa ni kuongezwa miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama),” alisema.

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alisema inahitajika bodi imara ya wakurugenzi na “kufuatwa sheria itakayoifanya TPA kubaki kuwa mwezeshaji na sio mtendaji.”


Zitto, ambaye pia ni mtaalamu wa uchumi aliyewahi kuwa mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (PAC) likiwamo la TPA alisema, “sekta binafsi iendeshe bandari kama mwendeshaji.”

Pia, alisema Serikali inapaswa kuwapa nafasi wataalamu wa bandari kuwa watendaji, badala ya kuruhusu wasio na taaluma hiyo kuiongoza mamlaka hiyo.

Akizunguzia changamoto hizo, Mhandisi wa Mifumo, Nseya Kipilyango alisema mianya ya upotevu wa mapato, urasimu na msongamano wa magari bandarini hutokana na changamoto za kimifumo.

“Utabadilisha wakuu wa taasisi hata aje mtu kutoka mbinguni, lakini kama hakuna mifumo bora bado changamoto zitakuwepo kwa kuwa atakuja kufanya kulingana na mfumo unavyotaka,” alisema Mhandisi Kipilyango.


Pia, alisema mifumo ndiyo msingi mkuu wa uendeshaji wa taasisi na ukiimarishwa yeyote atakayeingia itamchukua muda mfupi kuendana nayo.

Selemani Kakoso, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu alisema, “kuboreshwa kwa mifumo ni jambo moja, lakini usimamizi wake ni suala lingine muhimu linahitaji kuzingatiwa.

“Itumike mifumo ya kielektroniki, hii itakuwa mwarobaini wa changamoto zinazojitokeza, tukitumia mifumo ya ‘manual’ inashawishi watu kufanya ubadhirifu.”

Miaka 10 ya moto

Kabla ya Hamissi, mwaka 2012 mamlaka hiyo ilikuwa inaongozwa na Ephraim Mgawe, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu, ambaye aliondolewa katika nafasi hiyo Agosti 23, 2012 baada ya tuhuma zilizoibuliwa na tume iliyoundwa na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe.


Miongoni mwa tuhuma zilizokuwa zikimkabili ni pamoja na kushuka kwa mapato ya bandari kutoka Sh36 bilioni ya mwaka 2011 hadi kuwa Sh23 bilioni.

Baada ya sekeseke hilo, nafasi ya ukurugenzi ilikaimiwa na Madeni Kipande, ambaye Februari 16, 2015 alisimamishwa kazi na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wakati huo, Samwel Sitta.

Awadh Massawe aliachiwa kijiti kukaimu nafasi hiyo na baadaye Oktoba 18, 2015 aliyekuwa Rais wakati huo, Jakaya Kikwete alimteua kuwa mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo.

Nafasi hiyo alidumu nayo kwa miezi mitatu tu na baadaye Desemba 7, 2015 ilikoma kwa kutumbuliwa yeye, mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TPA, Profesa Joseph Mchambisaka na Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaban Mwinjaka.

Huo ulikuwa utawala mpya chini ya Hayati John Magufuli, ambaye alitaja sababu za kuwatumbua ni kuwepo kwa mianya ya upitishaji mizigo bila utaratibu katika bandari hiyo.


Baada ya vuguvugu hilo aliteuliwa Deusdedith Kakoko aliyekaimishwa wadhifa kuanzia Juni 25, 2016 akitokea Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na baadaye kuteuliwa katika nafasi hiyo mwaka 2018.

Hata hivyo, naye hakudumu mamlakani kwa tuhuma mbalimbali, ikiwamo ubadhirifu wa fedha na kuwekwa kando Machi 28 mwaka jana ili kupisha uchunguzi.

Baada ya hapo aliteuliwa mkurugenzi mpya wa mamlaka hiyo Erick Hamissi, ambaye naye ametenguliwa.Nafasi za Ajira Jiunge na Ajira Yako Telegram Group

 CLICK HERE


Post a Comment

0 Comments