Kiungo mshambuliaji wa Klabu ya Yanga, Aziz Stephanie Ki amesema kuwa kikosi cha timu hiyo msimu huu ni bora zaidi kuliko msimu uliopita kwani wameanza vizuri kwenye mechi zao na kila mmoja ana uwezo wa kufunga badala ya kumtegemea mchezaji mmoja.
Aziz Ki amesema hayo kuelekea mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al-Merrikh ya Sudan itakayopigwa kesho Septemba 30, 2023 katika dimba la Azam Complex, Chamazi.
Katika mechi tatu za Ligi, Yanga imeshinda mechi zote ikiwa imefunga mabao 11 bila kuruhusu bao hata moja wakati kwenye Ligi ya mabingwa, katika mechi tatu wamefunga mabao 9, na kuruhusu bao 1 pekee.
“Siwezi kuwaahidi lolote mashabiki kwa sababu hujui lolote kuhusu kesho, lakini jambo la muhimu ni kujituma kwa sababu timu ilinisajili kwa kuwa inataka kuingia hatua ya makundi. Msimu uliopita haikuwezekana lakini tunamshukuru Mungu.
“Huu msimu timu yetu iko imara zaidi ya msimu uliopita kwa ninavyoiona mimi. Kila mchezaji anacheza vizuri kwa hiyo tunaamini timu itashinda na kwenda makundi lakini kila mchezaji anatakiwa kujituma kwanza uwanjani.
“Jambo pekee ninaloweza kuwaahidi Wananchi ni kwamba nitaingia uwanjani na kujituma kwa asilimia 100 ili kuipa ushindi timu yangu,” amesema Aziz Ki
Nafasi za Ajira Zilizotangazwa Leo na Makampuni Bonyeza HAPA