Kinachotokea Iringa, Tafsiri Yangu.

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

Ndugu zangu,

Leo saa mbili na nusu asubuhi nilifika Jengo la NSSF nikitokea kufanya jogging yangu ya asubuhi. Nilifika hapo kuwahi kununua magazeti.

Hali ilikuwa shwari kama ilivyo kawaida ya Iringa Jumapili asubuhi. Kunako saa tatu asubuhi nilipokuwa nyumbani nikisoma magazeti, ndipo niliposikia mlio wa kwanza wa bomu la machozi. Idadi yake ikaanza kuongezeka.

Nikiwa na kamera yangu nikajisogeza hadi katikati ya mji kufahamu zaidi kinachotokea. Nilichokiona ni vurugu kati ya Wamachinga na Jeshi la Polisi.

Tatizo?

Ni dogo sana, lakini linakuzwa kwa vile siasa imepelekwa mbele badala ya kutanguliza hekima na busara. Kwa kufuatilia suala la Wamachinga kufanya biashara eneo la barabarani pale Mashine tatu naamini kabisa, kuwa Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Msigwa angeweza kuepusha hali inayoendelea sasa kwa kuwasihi Wamachinga watii kwanza amri ya Manispaa, na yeye, kama Mbunge wao, kujiingiza kwenye mazungumzo ya dhati na wenzake kwenye Halamshauri ya Manispaa ya Iringa katika kutafuta ufumbuzi wa suala hili. Na hiyo ndio siasa. Siasa ina maana ya majidiliano endelevu badala ya kuhamasisha matumizi ya nguvu au vurugu pale milango ya majadiliano ingali wazi.

Kinachotokea Iringa kwa sasa ni doa kubwa kwa mji wetu wenye sifa ya muda mrefu ya utulivu. Kina athari kubwa kiuchumi pia. Pale Iringa mjini nilichokiona leo ni kama mji ulio katika mapigano ya kivita. Watu ni wachache na wenye hofu.

Biashara nyingi zimesimama. Niliziona Daladala zikitoka Kituo cha Miyomboni bila hata abiria, watoke wapi? Wakati kwa sasa walio nje ya mji wameambiwa na jamaa zao walio katikati ya mji kuwa wasijaribu kufika mjini, kwamba hali imechafuka.

Nimeongea na mwuza nyama ya bucha aliyeniambia kuwa mgomo wa Daladala wa hivi karibuni ulimfanya apate hasara kubwa kwenye biashara yake ya nyama kwa vile wateja wake wengi wanatoka nje ya mji. Na anachokiona leo ni hasara nyingine kwa vile hakutakuwa na biashara nzuri. Je, ni wafanyabiashara wangapi watakaoathirika na hali hii ya leo?

Na kwa kuwa mkweli, kisiasa kinachotokea Iringa kwa sasa kinaweza kuwa na athari hasi kwa Mchungaji Msigwa badala ya kumjenga kisiasa, kwani, wengi niliozungumza nao katikati ya mji wanamwona Mchungaji Msigwa kuwa ni mtu ambaye angeweza kuiepusha hali hii kama asingeyatumia majukwaa ya siasa kuwahamasisha Wamachinga kuendelea kufanya biashara, na hivyo, kutokutii amri ya Manispaa.

Mchungaji Msigwa ni rafiki yangu, muda mfupi uliopita nimempigia simu. Imeita bila majibu. Mmoja wa watu wake wa karibu ameniambia yuko kwenye Harambee pale Tumaini University.

Kama Mchungaji Msigwa angejibu simu yangu, basi, ningemwambia haya ninayoyaandika hapa.

Maggid Mjengwa,
Iringa.
0754 678 252
-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Wewe ni mmoja wa watu wachache wenye busara waliobaki TZ. Naomba usikate tamaa na ushuri wako.

    ReplyDelete

Top Post Ad