MWENYE MACHO HAAMBIWA TAZAMA EAST AFRICAN COMMUNITY INAKUFA

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

Mimi siku zote husema si nabii wala mbashiri, sina ujuzi wa kutembelea nyota, lakini kwa mambo yote ambayo ninayaona kwa sasa, hakika ni alama mbaya , hatari kwa nchi yangu, Tanzania.
Hakuna shaka, pia ni hakika kwamba ni hatari pia hata kwa uhai na ustawi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa jumla wake.
Inanikumbusha mwaka 1977 ambako EAC ya mwanzo ile ya kina Jomo Kenyatta, Dk Milton Obote na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilivunjika, ingawa safari hii suala la itikadi zinazokinzana haliwezi tena kuwa sababu au chanzo.
Kwa waliokuwa vijana au watu wazima zama hizo wanakumbuka jinsi EAC ya wakati ule ilivyovunjika na kuiacha kila nchi kati ya Tanzania, Kenya na Uganda ikichukua mali, madeni ya jumuiya hiyo na kila moja na msimamo wake, ikiendesha pia mambo yake kwa mgawanyo wa mali ambao haukuwa wa haki. Ni wazi kwamba juhudi za marais waliofuata, Daniel arap Moi (Kenya), Benjamin Mkapa (Tanzania) na Yoweri Museveni (Uganda) zikawezesha kurejea na kuzaliwa kwa EAC mpya, yenye makazi yake Arusha, mahali ambako kwa sasa zimewekezwa fedha lukuki kujenga makao makuu mapya, ingawa kwa sasa jumuiya hiyo inayumba, inatikisika.
Yaani, EAC ya sasa ambayo pia imejumuisha nchi za Rwanda na Burundi kama wanachama wake wapya, tayari inazo nyufa lukuki ambazo kwa mtazamo wangu zinaashiria kuanguka au kuporomoka kwake, huenda siku si nyingi.
Zipo kila dalili kwamba EAC yetu ya sasa ya wanasiasa, wasaka tonge wengi ambayo imekuwa na ndoto za kuwa jumuiya moja kubwa yenye nguvu kibiashara, kisiasa, ndoto zake hizo zimekwisha na tayari EAC imegawanyika katika makundi.
Makundi hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yanatokana na mitazamo ya kimasilahi  zaidi ya viongozi wakuu wa nchi tatu,  hasa Rwanda, Kenya na Uganda, kwa kweli yanaiacha EAC ya sasa katika hatari ya kufa kabla ya kutimiza malengo yake.
Ni bahati mbaya kwamba Burundi, nchi ambayo imekuwa katika mizozo mingi ya ndani, vita ya wenyewe kwa wenyewe, haina habari na kinachoendelea, haina upande katika mzozo huu wa sasa wa EAC.
Mzozo huu kwa macho ya mbali unaweza kuonekana kuwa baina ya Rais Jakaya Kikwete dhidi  ya Rais Paul Kagame wa Rwanda, wengine wanaingia kama mashabiki, makuwadi.
Inawezekana kuwa mzozo si baina ya wawili hao, Kikwete na Kagame, kwani huenda hata Kenya ya Rais Uhuru Kenyatta na Uganda ya Museveni zinaiona Tanzania kama tishio kwa masilahi yao. Hakuna shaka kwamba matarajio ya wengi kule Kenya kwa mfano kuifikiria Tanzania kama eneo la kuingia kiholela, kujichotea mali, ardhi, ajira kama wapendavyo kupitia EAC yanaonekana kukwama.
Uganda ya Museveni, nchi  ambayo siku zote ua mara nyingi  imekuwa ikitegemea magendo ya kahawa, maharage, ndizi kutoka Kagera kupitia njia za panya si vituo halali vya mpakani kama Mutukula au Murongo.
Huenda nayo inaona kwamba biashara hii kuwa si endelevu kama ilivyo pengine kwa kufanya biashara au ushirikiano  mzuri zaidi na Kenya kwa njia ya barabara, reli.


Ni dhahiri, Uganda na Kenya kwa sasa zinaelewana vizuri zaidi na hata kuaminiana kuliko ilivyo kwa Tanzania.
Ni vyema Watanzania muelewe kuwa Uganda ambayo haina bandari na siku zote hutegemea bandari zenu, kwa maana ya Dar es Salaam, Tanga na hata ile ya Mwanza kupitishia bidhaa zao, inaiona nchi yenu kama si mshirika mzuri na mwaminifu tena mwenye kuaminika. Huenda zipo sababu za kwa nini Waganda wamefikia mahali pa kufikiria hivyo dhidi ya nchi yetu ambayo imejidai kisiwa cha amani, utulivu kwa muda mrefu, hasa kama idara za umma kama TRA (Mamlaka za Mapato), bandari (TPA) hazikuwa makini, kuangalia ni nini kinachowakwaza wafanyabiashara au Serikali ya Uganda hadi wakachagua kuirudia Mombasa, Kenya badala ya Tanzania. Kama tatizo ni urasimu, uzembe, umangimeza kwenye mamlaka zetu, hakuna shaka kwamba huenda ndiyo unawafanya pia Wanyarwanda waichague bandari ya Mombasa, mahali ambako ni mbali zaidi si Dar es Salaam tena!
Kama kuna mtu anabisha, aangalie mifano hii michache ya mambo yale ambayo yanaendelea ndani ya EAC kwa sasa na ambayo yanatoa ishara wazi kwamba hali tena si shwari. Kwa siku za karibuni, viongozi wakuu wa Kenya, Uganda na Rwanda wamekutana mara kadhaa, wakizungumzia mambo makubwa kiuchumi, kisiasa lakini wakimwacha nje Rais Kikwete. Kwa nini?
Kana kwamba hiyo haitoshi, pia wamefanya mkutano wa uwekezaji kule Entebbe, Uganda, lakini mbona Tanzania ilisahaulika, jiulize ni nini sababu?
Ninadhani Tanzania kama ina macho itazame, Rais Kikwete na timu yake wakae chini , waangalie kama ni wema ambao nchi yetu imetenda kwenye ukanda huu,  imetunza wakimbizi,  inalinda usalama kule DRC, mahali ambako Rwanda, Uganda zinadaiwa kuwa na masilahi, azinduke.
Viongozi wetu, yaani mawaziri wa uchukuzi, ujenzi au hata mawasiliano, washtuke na kuona watendavyo Kenya, Uganda na Rwanda ambao wameanza ujenzi wa reli kati ya Mombasa-Kampala-Kigali, inayotarajiwa kumalizika mwaka 2018.
Tanzania ina nini cha kuendelea kukaa chini na kujidai kwamba inapigania ushirikiano wa EAC, inapanga reli ya Tanga- Musoma kwenda Uganda, mradi ambao upo kwenye makaratasi. Reli ya Isaka, Bujumbura- Kigali imebaki simulizi, tumekwisha! Hakuna shaka kwamba huu wa sasa ni urafiki wa shaka shaka,  hakuna tena ushirikiano wa dhati baina ya nchi hizi tatu waanzilishi wa EAC.
Hata hivyo, hili la Rais Kagame kuendelea kuchokonoana na Rais Kikwete, pia si dalili njema kwa ustawi wa EAC.
Kenya, Uganda zilizotegemea kuchuma fedha kutoka kwa abiria wa mabasi waendao Mwanza, Kagera kupitia Nairobi na Kampala, sasa zinalia baada ya sisi kujenga barabara nzuri za lami kutoka Dar es Salaam kwenda  Kanda ya Ziwa huenda ni wivu ni maendeleo kwa miundombinu yetu.
-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Ama kwa hakiaka ili umeliona kwani hata mimi niliwaza tatizo la Tanzania kutengwa na wanajumuia kama dalili za EAC kuvunjika tena/kwa mala nyingine, lakini bora kuvunjika kuliko kendelea nao kwani ushirikiano huu umekuwa wa kima shaka shaka sana na hii inachagizwa sana na taifa makubwa kufanya ziara hapa Tanzania. Heri kila mtu akaenda kimpango wake.

    ReplyDelete

Top Post Ad