WOSIA WA GURUMO WAZUA UTATA

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

Stori: Mayasa Mariwata na Andrew Carlos
MKONGWE wa muziki wa dansi nchini, Muhidin Mohamed Mwalimu Gurumo ‘Maalim Gurumo’ amezikwa jana kwenye makaburi ya kijijini kwake, Masaki, Kisarawe mkoani Pwani, lakini wosia aliouacha kuhusu mazishi yake umezua utata, Risasi Mchanganyiko limedokezwa na wengi.

Kwa mujibu wa chanzo, wakati wa uhai wake Maalim Gurumo ambaye alikuwa mwanamuziki wa bendi mbalimbali nchini, ikiwemo Ottu na baadaye Msondo Music Band, alisema atakapotangulia mbele ya haki asizikwe siku inayofuata.

LIMWAMBIA NANI?
Kwa mujibu wa chanzo, Gurumo alimpa wosia huo mjomba’ake aitwaye Selemani Mikole ambaye ndiye aliyemlea alipofika jijini Dar es Salaam baada ya kufiwa na baba yake mzazi, mzee Mohamed Mwalimu Gurumo.

“Gurumo alikataa kuzikwa siku inayofuata. Mjomba wake ndiye aliyetoa siri hiyo mara baada ya Gurumo kufariki dunia.

“Yaani alitaka hivi, mfano amefariki dunia leo (jana Jumanne) basi mazishi yake yawe baada ya siku mbili, yaani keshokutwa (Alhamisi).

“Mjomba’ake alimuuliza sababu ya uamuzi huo, akasema yeye ni mtu mwenye mashabiki wengi, angeomba pawe na muda ili wengi waweze kuhudhuria mazishi yake,” kilisema chanzo hicho.

WAISLAM WATOFAUTIANA
Jumatatu iliyopita kwenye msiba wa nguli huyo nyumbani kwake, Mabibo-Makuburi jijini Dar es Salaam baadhi ya waombolezaji wenye imani ya Kiislam walisikika wakipingana na wosia huo wa marehemu.

Baadhi walisema si sawa Muislam kuzikwa baada ya saa ishirini na nne huku wengine wakisema wosia wa marehemu ndiyo maelekezo makuu ya mazishi.

“Hapa hatuzungumzii sheria za dini, tunazungumzia kutii wosia wa marehemu. Siku zote wosia wa marehemu unazingatiwa kwanza,” alisikika akisema mwombolezaji mmoja baada ya kuambiwa mazishi ya marehemu huyo ni Jumanne na si Jumatatu kama alivyoamini.

UISLAM UNATAKAJE?
Risasi Mchanganyiko lilipata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya viongozi wa Kiislam wa jijini Dar es Salaam ambapo kila mmoja alitoa mwongozo wake anaoujua kuhusu imani ya Kiislam inavyosema kuhusu mazishi ya muumini wake.

“Kwenye Uislam kuna ngazi tatu tu baada ya kifo. Kuoshwa, kuswaliwa na kuzikwa. Kama mtu anakata roho asubuhi na madaktari wakathibitisha, mwili wake hautakiwi kulala,” alisema shehe mmoja huku akiomba kusitiriwa jina.

MAALIM HASSAN NAYE ALONGA
Risasi Mchanganyiko pia lilizungumza na mtabiri maarufu nchini kwa sasa, Hassan Hussein Yahya ‘Maalim Hassan’ ambaye kwa upande wake aliweka wazi mambo haya:

“Kusema kweli Uislam mwili haulali. Labda kama mtu amekutwa na mauti usiku, lakini siku inayofuata lazima akasitiriwe (akazikwe).

“Endapo kuna dharura sana, basi zisipite saa ishirini na nne tangu kifo. Lakini hilo la Gurumo sidhani kama ni tatizo, unajua imani ipo, lakini pia tunaheshimu mila na desturi zetu Waafrika.”


SHEHE MKUU MKOA WA DAR ES SAALAM
Gazeti hili pia lilizungumza na Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Musa Salum ambapo alisema:

“Katika Uislam hakuna sheria kwamba  mtu akifa lazima azikwa siku hiyohiyo, wala hakuna siku zilizotajwa kuwa ndizo za marehemu kuwepo kabla ya mazishi. Ila kumzika marehemu mapema ni suna.
“Mbona Mtume Mohamed (S.A.W) alikufa Jumatatu akazikwa Jumatano?”

KUMBE SI DHAMBI
Pia Risasi Mchanganyiko lilizungumza na baadhi ya Waislam wanye elimu ya imani hiyo kwa undani ambapo wengi walisema mwili wa marehemu kuzikwa ndani ya saa 24 ni sheria ya kawaida lakini si dhambi kama ikitokea ukapitiliza saa hizo.


ALIJITABIRIA KIFO?
Akizungumza na gazeti hili juzi kwa majonzi makubwa, mtoto wa marehemu aitwaye Mariam Gurumo alisema baba yake ni kama alijitabiria kifo kwani Aprili 9, mwaka huu (siku nne kabla ya kifo) walikwenda Kisarawe kwa ajili ya kusalimia ndugu, jamaa na marafiki na kurudi Dar.

“Hiyo safari ilikuwa niende mimi. Nikaenda nyumbani kumuaga, lakini akasema lazima twende familia yote. Basi tukajaza mafuta kwenye lile gari alilozawadiwa na Diamond (Toyota FunCargo) tukaenda.

“Tulipofika, baba akazua tukio jingine, akasema lazima tutembelee makaburi ya familia kwa ajili ya kuyasafisha na kupiga dua kuwaombea marehemu waliolala pale jambo ambalo kwetu sisi watoto tulilishangaa,” alisema mtoto huyo.


Akaendelea: “Lakini tulipojiandaa kwenda makaburini, mvua kubwa ilinyesha. Kwa hiyo tukamwacha baba tukaenda sisi kufanya shughuli hiyo.

TATIZO LAANZA HADI KIFO
Mtoto huyo aliendelea kuweka kwamba, wakati wanarudi kutokana na milima na mabonde ghafla hali ya mzee Gurumo ikawa mbaya. Walipofika Msanga akaomba kwenda kujisaidia. Mara mvua kubwa ikanyesha tena naye akanyeshewa na kulowa chapachapa.

Alisema kuwa, hali hiyo ilimsababishia mzee Gurumo kuzidi kudhoofu zaidi kutokana na tatizo la mapafu kubana na kushindwa kupumua sawasawa.

“Tulifika Dar, hali ikazidi kuwa mbaya ndipo ikatulazimu kumkimbiza Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu ambapo Jumapili akafariki dunia majira ya saa tisa alasiri,” alisema mtoto huyo.
GPL

-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Post a Comment

3 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. pumzika kwa aman

    ReplyDelete
  2. Bwana Ametwaa Bwana ametoa jina la Bwana liimidiwe.amina

    ReplyDelete
  3. RIP KAMANDA GURUMO, TUTAKUKUMBUKA DAIMA KWA NYIMBO ZAKO ZA KIAFRIKA

    ReplyDelete

Top Post Ad