Mapya Yaibuka Katika Ufisadi wa Fedha za IPTL

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

- Rugemalira amruka Seth kwa CAG
- Andrew Chenge ataka asihusishwe

MMOJA wa waliokuwa wamiliki wa Kampuni ya Independent Power (IPTL) amedai hana ushahidi na hakuhusishwa katika uuzaji wa hisa za mbia mwenzake wa kampuni hiyo, uuzaji ambao hatimaye umesababisha kuchotwa kwa mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Tegeta Escrow, imefahamika.

Mmiliki huyo ni Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering (VIPEM), James Rugemalira na alitoa maelezo hayo kwenye ofisi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo inachunguza tukio la kuchotwa kwa fedha hizo zilizokuwa zimehifadhiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Katika maelezo aliyoyatoa kwa CAG na ambayo Raia Mwema imefanikiwa kupata nakala yake, Rugemalira alieleza kwamba hakushirikishwa wakati mbia mwenzake wa zamani katika IPTL, Kampuni ya Mechmar ya Malaysia, ilipofanya uamuzi wa kuuza hisa zake (asilimia 70) kwa Kampuni ya Pan African Power Solution (PAP) ambayo sasa ndiyo inamiliki IPTL.

“Bwana Rugemalira hakuwa na ushahidi wa kuuzwa kwa hisa za Mechmar kwa PAP ingawa alikwishaona baadhi ya barua za Mechmar kwenda Wizara ya Nishati na Madini.

“Rugemalira hakuhusishwa katika uuzwaji wa Mechmar kwa Piper Link. Wakati wa kusaini transfer tarehe 24/1/2014, kuna document (nyaraka) Bwana Rugemalira aliiona ambayo inaonyesha kununuliwa kwa share (hisa) za Mechmar,” inasema sehemu ya maelezo hayo ya Rugemalira ambayo yamesainiwa naye Septemba 10, mwaka huu.

Rugemalira naye aliuza hisa zake kwa kampuni hiyo ya PAP inayomilikiwa na Harbinder Seth Singh kwa thamani ya dola za Marekani milioni 75 (sawa na shilingi bilioni 123 za Tanzania).

Uuzwaji wa hisa za Mechmar kwa Piper Link na hatimaye PAP, ndiyo uliosababisha Rugemalira auze hisa zake kwa kampuni hiyo; tukio ambalo mwisho wake umewezesha kutolewa kwa fedha katika akaunti ya Tegeta.

Katika maelezo yake kwa CAG, Rugemalira ameeleza kwamba kwa kadri anavyofahamu, alilipwa fedha hizo kwa taratibu halali za kibiashara na kisheria.

Ofisi ya CAG inafanya uchunguzi kutafuta ni kwa vipi kiasi cha shilingi bilioni 200 zilitolewa katika akaunti hiyo ya Tegeta iliyokuwa ikishikiliwa na BoT na kulipwa kwa PAP.

Pia alisisitiza katika maelezo yake hayo kwamba uamuzi wa serikali, akimtaja Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi, kuruhusu fedha hizo zitoke BoT na kumaliza mgogoro zimeiokoa serikali na hasara nyingi ikiwamo kununua umeme wa bei ghali zaidi kutoka sehemu nyingine.

Hata hivyo, maelezo hayo ya Rugemalira yamefunua mapya taarifa kuhusu uhalali hasa wa Singh kupewa hisa za Mechmar na hatimaye kuruhusiwa kuchukua fedha hizo zilizokuwa zimehifadhiwa BoT.

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo ndiyo iliyomwagiza CAG kufanya uchunguzi huo, ilikuwa na wasiwasi kwamba Singh atajipatia kiasi cha shilingi bilioni 200 kwa kununua hisa za Rugemalira.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, Piperlink ilinunua asilimia 70 ya hisa hizo za Mechmar kwa thamani sawa na shilingi milioni sita za Tanzania lakini nayo ikaziuza kwa PAP kwa thamani ya dola 300,000 (shilingi milioni 500 za Tanzania).

Hata hivyo, wakati Mechmar ikidaiwa kuuza hisa zake hizo mwaka 2010, taarifa zilizopo zinaonyesha kwamba ilikuwa imefilisiwa nchini Malaysia na kwa mujibu wa sheria za nchi za Jumuiya ya Madola, isingewezekana kuruhusiwa kuuza hisa zake.

“Ni kwa njia gani ambako PAP ilichukua hisa za Mechmar katika IPTL mwaka 2010 wakati Mechmar ikiwa inafilisiwa? Sheria za nchi zote ulimwenguni haziruhusu jambo hilo kutokea kwani ni marufuku hisa za kampuni iliyo chini ya muflisi kuuzwa au kufanyiwa biashara yeyote.

“Au, kama wengine wanavyoamini, wakurugenzi wa Mechmar waliwazidi akili wasimamizi wa Malaysia, ikiwa ni pamoja na Mahakama Kuu na kufaulu kuuza hisa zao? Anachoeleza Harbinder ni kuwa Mechmar kwanza iliuza hisa zake katika IPTL kwa kampuni kificho inayoitwa Piper Link, ambayo ilizihifadhi, kwa sababu moja au nyingine, huko British Virgin Islands vya Uingereza,” ilisema taarifa ya Kabwe iliyopelekwa kwa CAG, Machi mwaka huu.

Mmoja wa wabunge waliosimama kidete kutaka fedha zilizotolewa BoT zirudishwe, David Kafulila, alisema haingii akilini kwamba hisa ambazo zimenunuliwa kwa shilingi milioni sita na baadaye milioni 500, zipande thamani ghafla na kufikia mabilioni ya shilingi.

Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini (NCCR-Mageuzi), alisema suala la PAP kununua hisa za IPTL na hatimaye kupewa mabilioni hayo limegubikwa na rushwa.

Wakati hayo yakiendelea, zimeibuka tuhuma kwamba baadhi ya viongozi wa serikali wamepokea fedha kutoka kwa mmoja wa waliokuwa wamiliki wa IPTL katika mazingira ya kutia shaka.

Taarifa hizo zimeenea katika mitandao mbalimbali ya kijamii huku majina kadhaa ya viongozi wa serikali na wabunge yakitajwa.

Mmoja wa wabunge ambao majina yao yametajwa sana ni Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge, ambaye katika mazungumzo yake na gazeti hili amekataa kuzungumzia suala hilo.

“Mimi kwa sasa nashughulika na masuala ya Katiba. Nafanya kazi hadi usiku. Sipendi kujadili mambo yangu binafsi au ya kikazi na vyombo vya habari. Naomba kwenye suala hilo la IPTL mniache,” alisema Chenge.

Chenge ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa Katiba ya Bunge la Maalumu la Katiba linaloendelea na vikao vyake mkoani Dodoma.

Chanzo: Raia Mwema
----

Love Story ya NJIA PANDA,Ni Kali mnoo Jamani.

Kusikiliza au kusoma mwendelezo wake Tembelea www.makapedia.com kisha bofya palipoandikwa NJIA PANDA kila siku saa moja kamili jioni BURE au bofya HAPA

Pia Bofya HAPA kujiunga na what's app channel yetu,tukukumbushe kila siku.


-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad