Ukomo wa Urais wa Dk Shein Zanzibar Utata Mtupu

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

Ukomo wa madaraka wa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein umeibua utata na kusababisha wanasheria na polisi kutoa tafsiri zinazokinzana.

Wakati Chama cha Wanasheria wa Zanzibar (ZLS) kikisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar tarehe ya mwisho ya Dk Shein kuingia ofisini ni leo Novemba 2, polisi kwa upande wao wanasema Rais huyo anatakiwa kushika madaraka hayo hadi pale rais mpya atakapoapishwa.

Rais wa ZLS, Awadh Ali Said alisema mwishoni mwa wiki kuwa moja ya athari za tamko la Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta uchaguzi wa Zanzibar ni kusababisha mgogoro wa kikatiba hasa katika muda wa rais kushika madaraka.

Said alisema Ibara ya 28 (2) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 inaeleza kuwa Rais ataacha madaraka yake baada ya kumalizika miaka mitano kuanzia tarehe alipokula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kuwa Rais.

Alisema tafsiri yake ni kuwa tangu Dk Shein alipokula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kuwa rais Novemba 3, 2010 atakuwa ametimiza miaka mitano Novemba 2, 2015.

“Hivyo akiendelea kushikilia madaraka ya urais zaidi ya tarehe hiyo itakuwa kinyume na Katiba ya nchi,” alisema.

Kutokana na madai hayo, Jeshi la Polisi Zanzibar limewatahadharisha wananchi kutojihusisha na vitendo vya fujo kwa madai kwamba kuanzia leo hakutakuwa na Serikali.



Walichosema ZLS

Kwa mujibu wa Rais wa ZLS, maudhui ya Ibara 28 (1) hiyo ni kumpa uwezo wa kikatiba Rais kuendelea ili kutoa nafasi ya maandalizi ya kula kiapo kwa Rais anayefuata tu na si kuendelea kukaa madarakani bila ya kufanyika kwa uchaguzi au kwa sababu ya Uchaguzi kufutwa.

Hata hivyo Said alisema nchi kuendeshwa muda mrefu bila ya Baraza la Wawakilishi (MBW) kama mazingira yaliyopo yanavyoonyesha ni tatizo.

Alisema Katiba ya Zanzibar imeruhusu hali ya kuendesha nchi bila ya BLW kwa muda usiozidi siku tisini (90) tu kuanzia siku Baraza lilipovunjwa.

“Kwa mazingira tuliyonayo, siku tisini (90) zinazokubalika kikatiba zinaishia Novemba 12, 2015 kwa kuwa BLW lilivunjwa Agosti 13, 2015,” alisema.

Rais huyo wa TLS alionyesha pia hatari ya kuwa na rais ambaye yuko juu ya Sheria na Katiba, akibainisha Ibara ya 37 ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 inayoipa Mamlaka Baraza la Wawakilishi kuondoa kinga ya Rais kutoshtakiwa anapokuwa madarakani kama inavyotolewa na Ibara ya 36 ya Katiba.

Alisema katika mazingira yaliyopo hivi sasa ambapo ifikapo tarehe 12 Novemba, 2015, Baraza la Wawakilishi halitakuwapo na haliwezi kuitishwa kikatiba, ni wazi kuwa ikiwa Rais atafanya matendo yoyote yenye kuvunja katiba ya nchi na kukiuka kiapo chake, hakutakuwa na mamlaka nyingine yoyote yenye uwezo wa kuhoji matendo ya Rais.

Alidai hii inatoa fursa na inatengeneza hatari ya kuwa na Serikali inayoongozwa na ‘dikteta’.


Kauli ya Polisi

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame alisema jana kuwa kutokana na taarifa hizo za wanasiasa na watu wengine, huenda wananchi watakuwa huru kufanya watakavyo na hivyo kuvunja sheria.

“Tunawaomba wananchi kuacha ushabiki na jazba ili kuwaepusha na gharama za matatizo, wao wenyewe na familia zao. Waswahili wanasema ‘vyako ni vyako, likikupata ni la kwako na kila mchumia janga hula na mwanawe’,’’ alisema Kamishna Makame.

Makame alisema ni vyema kipindi hiki kuhubiri amani na kuwa na subira kuiachia ZEC ambayo ndiyo yenye dhamana na mamlaka ya kutangaza tarehe ya kurejewa kwa uchaguzi na si mtu mwingine.

Kamishna Makame alinukuu kifungu cha 28 (1) cha Katiba ambacho pia wanasheria wa ZLS walikitoa na kumwomba Rais wa Zanzibar kuchukua tahadhari ili asiwe wa kwanza kuvunja Katiba ya Zanzibar kwa kuvuka terehe ya mwisho kuwapo madarakani.

Kifungu cha 28 (1) cha Katiba kinasema, “Kufuatana na Katiba hii mtu ataendelea kuwa Rais mpaka (a) Rais anayefuata ale kiapo cha kuwa Rais, au (b)afariki wakati akiwa Rais, au (c) hapo atakapojiuzulu; au (d) iwapo amechaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ; au (e) kwa sababu yoyote nyingine ameacha kuwa kiongozi kwa mujibu wa vifungu vingine vya katiba hii.

“Ikumbukwe kuwa kutokuwapo Rais wa nchi kama inavyodaiwa, haimaanishi sheria hazipo na watu wafanye watakavyo. Kuna makosa ukiyafanya moja kwa moja sheria itachukua mkondo wake ikiwamo kufanya kitendo cha uvunjifu wa amani, kufanya maandamano au mikusanyiko ya watu isiyo halali,” alisema kamishna huyo.

 Lipumba: Ni jukumu la JK

Sakata hilo la Zanzibar kwa mara ya pili lilimwibua mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba akimtaka Rais Jakaya Kikwete kumaliza tatizo la Zanzibar kwa kuiamuru ZEC kumtangaza mshindi wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 ili kuliepusha Taifa lisiingie kwenye machafuko.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Lipumba alisema ni muhimu Kikwete akahakikisha anatekeleza hilo kabla ya kumaliza muda wake, badala ya kumwongezea matatizo na mzigo rais mpya, Dk John Magufuli anayetarajiwa kuapishwa Novemba 5.

“Alhamisi ijayo Dk John Magufuli ataapishwa kuwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Tanzania, Kikwete usimwongezee Magufuli matatizo, yaliyopo yanamtosha,” alisema Lipumba ambaye wiki iliyopita akizungumzia pia mgogoro huo akiitaka ZEC imtangaze mshindi.

Lipumba aliyepokewa na wafuasi zaidi ya 100 kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho, Buguruni , Dar es Salaam, alisema amelazimika kutoa ushauri huo baada ya kuona hatari iliyo mbele, iwapo wananchi wa Zanzibar watanyang’anywa haki yao.

“Vigogo wa Tanzania na Zanzibar wasisubiri hadi maafa yatokee ndipo waanze kuchukua hatua, watumie muda huu kuyazuia,” alisema na kuonya:

“Nayakumbuka mauaji ya wafuasi wa CUF yaliyotokea mwaka 2001 na wengine kukimbilia uhamishoni Shimoni nchini Kenya, nimeona kukaa kimya kutaleta madhara katika nchi hii,” alisema.

Mmoja wa wanachama wa chama hicho, tawi la Buguruni, Ashura Mohammed alisema ni muhimu Wazanzibari wapewe haki yao kwa matokeo ya uchaguzi walioufanya kutangazwa.

 ADC : Jecha, ZEC wamekosa sifa

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa chama cha ADC, Said Miraaj Abdulla amesema ZEC chini ya Jecha Salim Jecha haiwezi kusimamia tena uchaguzi wa Zanzibar baada ya siku 90 kwa sababu ina mapungufu mengi kama ilivyoyaainisha yenyewe.

Abdulla alisema sababu zilizotolewa na Jecha kufuta matokeo hazina mashiko, zimelenga kuficha ukweli na kutetea maslahi ya upande mmoja. Alisema chama chake kitasimamia haki na ukweli kuhakikisha kwamba matakwa ya wananchi yanasikilizwa.

“Kwanini Jecha aje leo kutueleza kuwa tume yake iliingiliwa na wanasiasa? Siku zote alikuwa wapi na alichukua hatua gani katika kuhakikisha tume yake inakuwa huru,” alihoji mwenyekiti huyo na kusisitiza kuwa kuna ajenda inafichwa na Jecha.

Mwenyekiti huyo aliendelea kusema, Jecha alisisitiza katika matamshi kwamba wajumbe wa ZEC walikuwa wamegawanyika kwa misingi ya vyama vyao lakini hakueleza ni kwa namna gani mgogoro wa wajumbe hao umeathiri kura zilizopigwa.

Aliwataka viongozi kuwa makini na matamshi yao ili yasije kusababisha migogoro na kuvunja amani ya nchi na vyama vyote kuwa na sauti moja ili viweze kutetea haki za wananchi wa Zanzibar ambao wamechagua viongozi wao kwa misingi ya kidemokrasia.

“Viongozi wa CUF na CCM waache kuangalia maslahi ya vyama vyao bali waangalie maslahi mapana ya umma. Chama changu kiko tayari kushirikiana na chama chochote katika kuhakikisha kwamba suluhu ya mgogoro huo inapatikana,” alisema.

Imeandikwa na Salma Said, Raymond Kaminyoge na Peter Elias

----

Love Story ya NJIA PANDA,Ni Kali mnoo Jamani.

Kusikiliza au kusoma mwendelezo wake Tembelea www.makapedia.com kisha bofya palipoandikwa NJIA PANDA kila siku saa moja kamili jioni BURE au bofya HAPA

Pia Bofya HAPA kujiunga na what's app channel yetu,tukukumbushe kila siku.


-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Tags

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. watanzania wapenda maendeleo tunasubiria kwa hamu kubwa kuapishwa kwa mheshimiwa seif shariff hamad kuwa rais wa zanzibar,tuna imani hili litafanyika wakati wowote kuanzia sasa.pili,watanzania tunasubiria kwa hamu kufikishwa mahakamanikwa aliyekuwa mwenyekiti wa ZEC jecha salum jecha kwa kufanya kosa kubwa la jinai kujitwalia madaraka ya zanzibar kwa kupindua kwa makusudi maudhui halisi ya uchaguzi mkuu upande wa mgombea urais zanzibar kwa kushindwa kumtangaza mshindi halali na badala yake kuiweka nchi katika rehani ya sintofahamu na machafuko.tatu orodha ya washitakiwa inaweza kuongezeka kadri mshtakiwa jecha atakavyoendelea kuhojiwa na polisi na vyombo vingine vya dola.

    ReplyDelete
  2. mumuache ariye changuriwa nawanaich aongoze jamani

    ReplyDelete

Top Post Ad