8/26/2020

Lindi: Mgombea Ubunge (Chadema) ‘Akamatwa Kwa Rushwa’
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Lindi imemkamata na inamshikilia mgombea ubunge wa Jimbo la Mtama kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Seleman Luwongo, kwa tuhuma ya kutaka kumpa rushwa ofisa uchaguzi wa halmashauri ya Mtama.


 


Akizungumza leo, Agosti 26, 2020, na waandishi wa habari mjini Lindi, mkuu wa TAKUKURU wa mkoa wa Lindi, Steven Chami, amesema taasisi hiyo inatarajia kumfikisha mahakamani Luwongo kwa tuhuma ya kutaka kumpa rushwa ya shilingi 1,540,000 ofisa uchaguzi wa Jimbo la Lindi ili atangazwe ameshinda wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi.


 


Chami alisema Luwongo alikamatwa jana jioni majira ya saa 12 huko Mtama. Alibainisha pia kwamba kiasi hicho cha fedha kilikuwa ni sehemu ya shilingi 10,000,000 za kuwahonga ofisa uchaguzi huyo na msimamizi wa uchaguzi wa Halmashauri ya Mtama ili atangazwe kuwa mshindi wa nafasi hiyo ya ubunge.


 


”Mtuhumiwa alikamatwa kufuatia taarifa iliyopokelewa ikieleza kuwa Agosti 21, 2020, majira ya saa tano asubuhi alikwenda katika ofisi ya uchaguzi pamoja na msimamizi wa uchaguzi ambapo lengo la maongezi yake ni kutaka asaidiwe kutangazwa mshindi wa kura za ubunge Jimbo la Mtama,” Chami alisisitiza.


 


Alibainisha kwamba  ili kutimiza lengo lake la kutangazwa mshindi Luwongo  aliandaa shilingi milioni 10 ili awape wote wawili (ofisa na msimamizi wa uchaguzi) na kwamba aliahidi  kutoa fedha za utangulizi siku ya kurejesha fomu.


 


Chami ambaye alikuwa sambamba na mkuu wa TAKUKURU wa mkoa wa Mtwara, Enock Ngailo, alisema baada ya uchunguzi TAKUKURU ilibaini pasipo nashaka kitendo kilichofanywa na Luwongo ni kushawishi kutoa rushwa.


 


Ameongeza kwamba hilo ni kosa kwa mujibu wa sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 kwa hiyo ofisi ya TAKUKURU ya mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na ofisi ya TAKUKURU ya Mkoa wa Mtwara ziliweka mtego uliomnasa Luwongo.


 


Chami alihitimisha kwa kusema kwamba baada ya kukamilisha uchunguzi, taasisi yake  inatarajiwa kumfikisha mahamani leo ili akajibu tuhuma inayomkabili kwa mujibu wa kifungu cha 15(1) (b) cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.


HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Weka Comment Yako Hapa Chini:
Share:
Loading...

0 [disqus]:

Post a comment

Click Below to Subscribe

Popular Posts

Loading...

Copyright © UDAKU SPECIAL BLOG | Powered by Blogger