8/07/2020

Wasanii Waliong’ara, Pumzi Ikakata


MUZIKI wa Bongo Fleva umekua ndani na nje ya Tanzania. Muziki huu sasa ni biashara kubwa mno, tofauti na miaka ya 2,000 ambapo wasanii waliishia kuwa maarufu tu, bila kupata kipato kikubwa kama miaka hii ya kuanzia 2010 hadi sasa.

Jambo la kushangaza na ambalo limemakinikiwa katika makala haya ni kwamba wasanii wengi wa Bongo Fleva huibuka na kung’ara zaidi kwa muda fulani kisha pumzi inakata na wengine hupotea kabisa.

Makala haya yanaangazia sababu za wasanii hao kuibuka, kung’ara, na kupotea.

Kwa upande mwingine makala hii pia inabainisha kuwa wasanii hao hupotea kwenye muziki kwa sababu mbalimbali;

Pamoja na kwamba utandawazi una faida nyingi mno kama vile kuufanya wimbo kuwa mkubwa na kupata mashabiki wengi zaidi kwa kuwafikia watu kwa njia nyingi na haraka, kujenga ushirikiano wa kimuziki urahisi na haraka kwa mataifa mengine, bado utandawazi huo unasababisha wasanii wa Bongo Fleva kuanguka na kushindwa kusimama tena kwenye muziki.

Baadhi ya wasanii baada ya kuwa kileleni, wanalewa sifa na kujikuta wakiendeshwa na utandawazi badala ya wao kuuendesha utandawazi huo.

Menejimenti ni kipengele kingine ambapo uongozi wa msanii unakuwa jukumu la kumsimamia msanii. Wako wasanii ambao kung’ara kwao kulitokana na menejimenti nzuri. Menejimenti ikiyumba inasababisha msanii kushuka kimuziki na hatimaye kupotea kabisa.

Kuyumba kwa menejimenti kunaweza kusababishwa na msanii mweyewe. Ifahamike kwamba umekuwa ni utamaduni wa wasanii kusimamiwa na menejimenti au watu fulani.

Ishu nyingine inayowaangusha wasanii wengi ni mabifu baina ya wasani. Hii ni sababu nyingine ya kuwavuruga kimuziki. Yapo baadhi ya makundi ya muziki yaliyosambaratika baada ya wasanii waliokuwa wakiyaunda kugombana wenyewe kwa wenyewe.

Ifahamike pia kwamba, popote penye migogoro hapawezi kuwa na maendeleo au mafanikio.

Wafuatao ni baadhi ya wasanii waliong’ara mno kitambo kisha pumzi ikakata na wengine kupotea kabisa;

Z-ANTO

Jina lake halisi ni Ally Mohammed, lakini jina la kutafutia ugali ni Z-Anto. Jamaa aliwika miaka ya 2,000 hasa alipoachia Ngoma ya Mpenzi Jini akiwa chini ya Lebo ya Tip Top Connection.

Z-Anto anasema kilichompoteza ni kuamua kuacha muziki baada ya kuvunja mkataba na Tip Top Connection. Anasema aliamua kuachana na muziki na kuendelea na mambo mengine ya biashara.

“Baada ya kuona hakuna faida ninayoipata, niliamua kuachana na mambo ya muziki na kuanza kufanya biashara zangu ili kumudu gharama za maisha yangu,” anasema Z-Anto.

NOORAH

Jina lake halisi ni Haji Nurah Ngarama. Ni maarufu zaidi kwa jina la Noorah au Baba Styles.

Jamaa ni miongoni mwa vichwa vikali mno aliyetokea kwenye Kundi la Chamber Squad lililokuwa na wasanii wakali kama marehemu Ngwair, Mez B na Dark Master.

Noorah alitamba mno miaka ya 2,000 na Ngoma ya Ice Cream.

Jamaa anasema sababu ya ukimya wake kwenye muziki ni kwamba kila jambo lina wakati wake hivyo kwa sasa ni kama sanaa imeshapita kwake kutokana na majukumu aliyonayo.

“Nimekaa kwenye tasnia ya muziki takriban miaka 10 hivyo najua muziki mzuri unavyotakiwa kuandaliwa, lakini kwa sasa sina muda huo, nina majukumu mengine,” anasema Noorah.

SOGGY DOG

Huyu ni lejendari mwingine wa Bongo Fleva. Jina la kutafutia ugali anafahamika kama Soggy Doggy, lakini kwenye kitambulisho cha Nida anajulikana kwa jina la Anselm Ngaiza. Ukimuita Chifu Rumanyika unakuwa hujakose. Ni miongoni mwa wanaharakati halisi wa muziki wa Bongo Fleva.

Soggy amewahi kutamba na mkwaju mkali wa Kibanda Cha Simu. Ni ngoma ambayo ina zaidi ya miaka 13, lakini bado haijachuja.

Jamaa ni miongoni mwa wasanii ambao wameamua kuikacha Bongo Fleva.

MARLAW

Huwezi kutaja orodha ya wasanii waliokubalika kwenye Bongo Fleva mwanzoni mwa miaka ya 2,000 bila kulitaja jina la Lawrence Marima Madole ‘Marlaw’.

Marlaw alikuwa jamaa mmoja hivi kutokea Iringa ambaye alitikisa vilivyo na ngoma kibao kama Rita, Daima Milele, Bembeleza, Mbayuwayu, Busu la Pinki, Pii Pii (Missing My baby) na nyingine kibao.

Kwa muda mrefu, Marlaw amekuwa kimya kwenye gemu. Kuna kipindi aliachia ngoma ambayo haikuwa kali kivile, akapotea na kuendelea na shughuli nyingine za kijamii.

JUMA NATURE

Huyu ni mkongwe mwingine kwenye Bongo Fleva. Anaitwa Juma Kassim ‘Nature’. Ni msanii ambaye amekuwa ana albam nyingi kwa mfululizo. Alianza kuachia Nini Chanzo (2001), Ugali (2003), Ubinadamu Kazi (2005) na Zote History (2006). Amewahi kufanya mambo makubwa kwenye muziki wa Hip Hop ambapo alikuwa mfano wa kuigwa na wasanii wengine wanaopenda muziki huo.

MR NICE

Msanii liyewahi kubamba na staili yake ya Tanzania, Kenya na Uganda (Takeu), Lucas Mkenda ‘Mr Nice’

Ni miongoni mwa wasanii walioutendea haki muzuki wa Bongo Fleva miaka ya 2,000. Ulikuwa ukipita kila kona lazima usikie muziki wake.

Alijizolea umaarufu mkubwa kuanzia kwa watoto hadi kwa watu wazima, lakini Mr Nice alikuja kupotea ghafla kwenye muziki, jambo liliibua sintofahamu kwa baadhi ya mashabiki wake.

WENGINE

Wengine waliong’ara na kupotea ni MB Dog, 20 Percent, Biz Man, Bwana Misosi, Mad Ice na wengine kibao.

MAKALA: KHADIJA BAKARI
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Weka Comment Yako Hapa Chini:
Share:
Loading...

0 [disqus]:

Post a comment

Featured post

Tovuti bora zaidi ya utabiri wa Soka Tanzania inakutuza shati ya Alex Iwobi iliyotiwa sahihi.

Jiunge nasi ili uweze kuweka dau kama mtaalamu na kubeti Ligi ya England, La Liga, ikiwemo jackpot. Tunakupa habari za mpira wa miguu na ...

Click Below to Subscribe

Popular Posts

Loading...

Copyright © UDAKU SPECIAL BLOG | Powered by Blogger