9/01/2020

Maofisa Benki, BRELA Kizimbani Kwa Kughushi Dola 300,000RAIA wawili wa kigeni, wafanyakazi wawili wa benki ya Equity na Msajili Msaidizi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka 13 likiwemo la kughushi na kutakatisha Dola za Marekani 300,000.

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa jana mahakamani hapo na wakili wa serikali mwandamizi, Wankyo Simon, imewataja washtakiwa hao kuwa ni, Mohammed Nur (48) raia wa Afrika Kusini, Umulkher Mohammed (34) raia wa Somalia, wote wafanyabiashara na Noel Shani (44) mfanyakazi Brela.

Wengine ni wafanyakazi wa benki, Alex Ndondole (33) na Emma Chikaonda ambaye hakuwepo mahakamani. Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu imedaiwa kati ya Machi 2011 na Mei 30, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao wote walikula njama kufanya kosa la kujipatia fedha kwa udanganyifu.

Katika shtaka la pili, mshtakiwa Nur na Mohamedi, wanadaiwa kughushi maamuzi ya bodi ya Kampuni ya Alliance Cargo Handling Ltd ya Februari 8,2014 kuonyesha kuwa kampuni hiyo imekubaliana kufungua akaunti katika Benki ya Equity tawi la Prestige wakati si kweli.

Wakili Wankyo amedai katika shtaka la tatu kuwa, Aprili 12, 2015 washtakiwa Nur na Mohamedi, walighushi maamuzi ya bodi ya Aprili 12, 2015 wakionyesha kwamba bodi imekubali kufungua akaunti Benki ya Amana Tawi la Nyerere Road huku wakijua kuwa siyo kweli.

Pia inadaiwa, Aprili 18 mwaka 2011 washtakiwa hao walighushi barua kuonyesha kuwa imetolewa na Brela kwa kuonyesha kwamba Mohammed ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Alliance huku akijua si kweli.

Aidha katika shtaka la tano mshtakiwa hao hao, Nur na Mohamed, wanadaiwa kughushi maamuzi ya bodi ya Machi 5, 2016 wakionesha Kampuni ya Alliance inabadili jina kutoka Alliance Cargo kwenda Africa Flight Service Tanzania wakati si kweli

Februari 8, 2014 mshtakiwa Nur aliwasilisha nyaraka ya uongo ya maamuzi ya bodi kuonyesha kwamba wamekubali kufungua akaunti Equity Banki huku katika shtaka la saba mshtakiwa huyo aliwasilisha nyaraka Amana Bank kuonyesha kuwa kampuni imekubaliana kufungua akaunti.

Aidha mshtakiwa Nur anadaiwa kuwasilisha Brela nyaraka kuonyesha wamekubaliana kubadilisha jina la kampuni huku wakijua kuwa siyo kweli.

Katika shtaka la tisa, inadaiwa Februari 10,2014 maeneo ya Equity Bank, mshtakiwa Nur na Mohamed kwa nia ya kufanya udanganyifu katika akaunti ya Kampuni ya Cargo iliyopo Equity, kwa udanganyifu walichukua mkopo wa Dola 300,000.

Wankyo alidai shtaka la 11, mshtakiwa tatu akiwa Msajili Msaidizi Brela anadaiwa kushindwa kuzuia uhalifu huku katika shtaka la 12 na 13 washtakiwa wote wanadaiwa kutakatisha Dola 300,000.

Hata hivyo, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.

Pia wakili Wankyo aliomba washtakiwa hao warudishiwe polisi kwa kuwa bado hawajapimwa iwapo wana maambukizi ya virusi vya corona au la, ombi ambalo mahakama iliridhia kwa ajili ya vipimo na kesi itatajwa Septemba 7 mwaka huu.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Weka Comment Yako Hapa Chini:
Share:
Loading...

0 [disqus]:

Post a comment

Click Below to Subscribe

Popular Posts

Loading...

Copyright © UDAKU SPECIAL BLOG | Powered by Blogger