Ticker

6/recent/ticker-posts
.

Bei Ya Petroli, Dizeli Yaongezeka

 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA  KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO BURE

 


 MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imebainisha kuwa bei za rejareja na jumla za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka mwezi huu ikilinganishwa na mwezi uliopita.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Gerald Maganga bei ya rejareja kwa petroli imeongezeka Sh 94 kwa lita sawa na asilimia 4.99, dizeli Sh 82 kwa lita sawa na asilimia 4.47 na mafuta ya taa Sh 94 sawa na asilimia 5.34, mtawalia.

Alisema ikilinganishwa na toleo la Februari, mwaka huu bei za jumla za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka kwa Sh 93.77 kwa lita sawa na asilimia 5.33, Sh 81.38 kwa lita sawa na asilimia 4.78 na Sh 94.16 kwa lita sawa na asilimia 5.74, mtawalia.

“Kwa Machi 2021, bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli na dizeli kwa Mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara) zimeongezeka ikilinganishwa na bei zilizotolewa Februari 3, mwaka huu,” alisema Maganga.

Alisema mwezi huu, bei za rejareja za petroli na dizeli zimeongezeka kwa Sh 163 kwa lita sawa na asilimia 8.47 na Sh 85 kwa lita sawa na asilimia 4.64, mtawalia.

Alisema, pia ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za petroli na dizeli zimeongezeka kwa Sh162.12 kwa lita sawa na asilimia 9.05 na Sh 84.80 kwa lita sawa na asilimia 4.97mtawalia.

“Hata hivyo, bei za mafuta ya taa hazina mabadiliko na zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo la Februari 3, mwaka huu. Hii ni kwa sababu, kwa Februari hakuna shehena ya mafuta ya taa iliyopokelewa kupitia bandari ya Tanga,” alieleza.

Kaimu mkurugenzi huyo alisema mwezi huu, bei za rejareja na jumla kwa bidhaa za mafuta ya petroli na dizeli kwa Mikoa ya Kusini (Mtwara, Lindi na Ruvuma) zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa mwezi uliopita kwa sababu hakuna shehena ya mafuta iliyopokelewa kupitia bandari ya Mtwara.

Alifafanua kuwa mabadiliko hayo ya bei yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji). Alisema bei hizo mpya zilizopanda zimeanza kutumika kuanzia Machi 3, mwaka huu.

Hata hivyo, aliukumbusha umma kuwa bei kikomo za bidhaa za

mafuta ya petroli kwa eneo husika zinapatikana pia kupitia simu za

mkononi kwa kupiga namba *152*00# na kisha kufuata maelekezo.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015 Kifungu Namba 166, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko.

“Ewura itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta. Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta,” alisisitiza.

Alisema kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ili mradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo kama ilivyokokotolewa na kanuni iliyopitishwa na Ewura na iliyochapishwa katika Gazeti la Serikali Namba 656 la Agosti 21 mwaka 2020.

Alisema vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango, yanayoonekana bayana na yakionesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika.

“Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja. Adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika,” alisisitiza.

Post a Comment

0 Comments