Bunge Lajadili Malori Kukwama Bandarini Dar

 


Bunge la Tanzania limeahirisha mjadala wa Wizara ya Afya kwa takribani nusu saa ili kujadili sakata la  malori kutoshusha wala kupakia mizigo kwa muda wa siku tano katika Bandari ya Dar es Salaam.

Hoja ya kuahirishwa kwa mjadala imewasilishwa leo Jumatano Mei 12,  2021 na mbunge wa Mafinga Mjini (CCM),  Cosato Chumi.

Chumi amesema Bandari hiyo ndio chanzo kikubwa cha kuendeleza nchi na kufanikisha miradi, “malori hayashushi wala kupakia mizigo kwa maana uchumi kwa namna fulani umesimama. Na tunazungumzia ushindani kati ya bandari yetu na nchi jirani.”

“Katika hali hii hatuwezi kukaa kimya  na kuacha mambo ya namna hii yaendelee ndio maana ninajenga hoja tuahirishe mjadala ili tujadili jambo hili nyeti.”

Amesema kuna mizigo inayokwenda kwenye miradi mbalimbali ikiwemo wa uzalishaji wa umeme wa maji  katika bwawa la mwalimu Nyerere na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), lakini imekwama katika bandari hiyo.

Amesema mizigo inayokwenda nchi jirani imekwama wakati Taifa linatarajia bandari hiyo kuwa na ushindani.

Baada ya hoja hiyo, Naibu Spika Dk Tulia Ackson aliruhusu hoja hiyo ijadiliwe kwa muda wa dakika 20 ambapo wabunge saba walipata nafasi ya kuchangia.

Akijibu Waziri wa Nchi  Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu,  Jenista Mhagama amesema tayari Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa amekwenda Dar es Salaam kushughulikia suala hilo.

 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA  KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO BURE