.

8/11/2021

Simbachawene: Magereza ya Tanzania Yanaendeshwa Kikoloni

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene amesema Magereza ya Tanzania yana viashiria vya ukoloni na kwamba kuna safari ndefu ya kuyabadilisha ili wahalifu watendewe haki za binadamu.

 

Kauli ya Waziri Simbachawene imekuja wakati kukiwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanaharakati wa haki za binadamu na wanasiasa wakidai kuwepo kwa vitendo vya ukatili ndani ya magereza.

 

Waziri Simbachawene ameyasema hayo mwisho wa wiki jijini Dar es Salaam, alipokuwa mgeni rasmi katika shughuli ya kuchangisha fedha za asasi ya kiraia ya Utu Kwanza (Consciousness for Humanity), akisema binadamu wanastahili heshima hata wanapokuwa magerezani.

 

“Magereza na masuala ya jinai, bado yana vi-elements (viashiria) vya kikoloni. Mfumo wake, na ukikuta gereza ambalo lina kiongozi anayesimama kwenye misingi ya kikoloni ya kizamani anapata nafasi kubwa na huyu ndiye anayeonekana anafanya kazi vizuri,” amesema Simbachawene.

 

Huku akifafanua umuhimu wa haki za binadamu kwa watu wote, Simbachawene amesema mtu kuwepo gerezani ni utaratibu wa sheria, hivyo sheria hizo zinapaswa ziendane na hali na hadhi ya maendeleo ya binadamu.

 

“Nikiri na nikubali, kwamba bado tuna safari ndefu ya kufanya katika kuleta mabadiliko ya kushughulika na uhalifu na wahalifu, lakini na sambamba na kuheshimu haki na utu wa binadamu.”

 

Ameendelea; “Wale maofisa wa magereza na askari wanaokiuka taratibu ni wale ambao dhamira na moyoni mwao wanasutwa, kwamba hawa ni binadamu wanapaswa kutendewa haki na utakuta sheria haziwaruhusu.”

 

Kutokana na hali hiyo kuna haja ya kufanya mabadiliko, huku akitaka wadau kusaidia mabadiliko hayo. “Kwa hiyo ipo haja kama Waziri ninayesimamia wizara inayosimamia magereza pamoja na sekta nyingine. Ipo haja ya kushirikiana na wadau kupitia forums (majukwaa) mbalimbali, likiwemo hili ambalo nimepata bahati na sikujua ina nini ndani yake,” amesema.

 

Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imempa maelekezo mahsusi ya mabadiliko hayo.

 

“Masuala ya jinai yana misingi yake na mtu hawezi akapewa adhabu mpaka awe amethibitika pasina shaka kwamba, ametenda kosa hilo. Kwa hiyo ni masuala mtambuka, ipo idara ya Mahakama, wapo wanaoendesha mashitaka, wapo wanaopeleleza kwa ujumla wake hao kuna kazi ya kufanya,” amesema Simbachawene.


HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:

0 Blogger:

Post a Comment

New Video - Wana Wanywe Pombe

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger