Ticker

6/recent/ticker-posts

Shahidi Kesi ya Kina Sabaya Adai Kuelekezwa Kusema Uongo na Wakili wake Mahakamani

 Habari Kama Hizi Zinapatikana UDAKU SPECIAL App, Download HAPA Bure: Link here>>>


Arusha. Shahidi wa saba upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya,Watson Mwahomange (27) amedai mahakamani kuwa wakili wake alimfundisha kusema uongo mahakama kwa kukana taarifa zake wakati akisomewa maelezo ya awali.


 Mwahomange ametoa madai hayo leo Jumanne Machi 15, 2022 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Patricia Kisinda wakati akiulizwa maswali na wakili wa utetezi Mosses Mahuna.


Mwahomange ambaye pia ni mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo, amekuwa akijitetea mwenyewe baada ya wakili wake kujitoa.


Amesema kuwa wakili wake alimueleza endapo atakubali atapewa adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela na kwamba, Juni 19, 2021 waliposomewa maelezo ya awali, alikataa maelezo yote aliyosomewa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Felix Kwetukia na kukubali maelezo ya kukamatwa na kufikishwa mahakamani tu.


Amedai kuwa alikataa kila alichoulizwa ikiwemo majina yake, umri wake, kabila lake na mashtaka yanayomkabili ila anachokisema kwa sasa chini ya kiapo ndiyo ukweli ikiwemo kukiri majina yake umri na kabila lake.


"Wakili wangu Fridolin Bwemelo aliniambia nikatae kila kitu kwani nikikubali nitafungwa ila kwa sasa niko chini ya kiapo ndiyo kinanizuia nisiseme uongo," amesema shahidi huyo.


ADVERTISEMENT

Sehemu ya mahojiano hayo ilikuwa kama ifuatavyo;


Wakili: Shahidi unaweza kuikumbusha mahakama majina yako


Shahidi: Watson Stanley Mwahomange na Henrick ni jina langu la ubatizo


Wakili:Ni sahihi licha ya majina hayo nyumbani kwenu unapoishi wanakuita Watii?


Shahidi: Ni sahihi maana ni kifupi cha Watson


Wakili: Sasa Bwana Watii kwanini uliacha shule form two??


Shahidi: Sikuishia Form two niliishia darasa la saba


Wakili: Shule gani?


Shahidi: Trust St.Patrick


Wakili: Kwa nini uliishia darasa la saba?


Shahidi: Nilipata matatizo (ajali) nikaacha shule


Wakili: Kwa nini hukwenda shule?


Shahidi: Nilikuwa na talent ya kupiga picha nilijifunza kupitia nilìokuwa nakaa nao


Wakili:Ulijifunza wapi uongo?


Shahidi:Uongo sijawahi kufundishwa popote


Wakili: Ni kipaji?


Shahidi: Sijui


Wakili: Ni kweli 4/6/2021 uliletwa mahakamani na kushitakiwa kwa makosa mawili? Kuunda genge na kutakatisha fedha


Shahidi: Ni kweli


Wakili: Wakati unasomewa makosa hayo 4/6/2021 wewe ulikuwa unamfahamu Sabaya?


Shahidi: Ndiyo


Wakili: Sylvester?


Shahidi:Ndiyo


Wakili: Enock?


Shahidi:Ndiyo


Wakili:Ni kweli kwamba 16/9/2021 hapa mahakamani ulisomewa maelezo ya awali hapa mahakamani?


Shahidi:Ndiyo


Wakili: Ni kweli kwamba kati ya maelezo yote yaliyosomwa na Wakili wa Jamhuri Felix Kwetukia wewe ulikataa maelezo yote ukakubali kukamatwa na kufikishwa mahakamani?


Shahidi: Ndiyo nilikataa pamoja na jina


Wakili:Ulikataa yote


Shahidi: Hayo yalikuwa maelekezo ya wakili wangu aliniambia nikatae kila kitu


Wakili:Ni kweli kwamba ulikataa jina lako, umri wako, ulikataa kabila, ulikataa makazi yako katika hayo maelezo yaliyosomwa na wakili wa Jamhuri?


Shahidi:Ni kweli nilikataa


Wakili: Jana na leo umeieleza hii Mahakama unaitwa Watson Stanley Mwahomange lakini ni sahihi jina hilo ulilikataa


Shahidi: Nililikataa kwa maelekezo ya wakili


Wakili: Wakili wako alikuwa nani?


Shahidi: Wakili ninayemjua alikuwa Fridolin


Wakili: Ulikataa umri wa miaka 27 jana ukaeleza mahakama wewe una umri wa miaka 27


Shahidi: Ni kweli


Wakili: Lakini ni kweli tarehe 16/9/2021 ulikataa?


Shahidi: Sikuwa chini ya kiapo.Nilikataa kwa maelekezo ya wakili wangu aliniambia nitafungwa


Wakili:Ni kweli kwamba ulisomewa facts zinazosema wewe unafahamiana na wenzako sita unaoshtakiwa nao ukakataa


Shahidi: Niliambiwa na Wakili niseme hivyo


Wakili: Je ni kweli ulisema hivyo?


Shahidi: Sikumbuki ila wakili aliniambia utakachokubali utafungwa usije kukubali


Wakili: Ikawaje jana ukasema unawafahamu Sabaya, Enock na  Sylvester


Shahidi: Ningekuwa siwafahamu nisingekamatwa nao na jana nilikuwa chini ya kiapo


Wakili: Kwa hiyo wewe Wakili akikuambia sema uongo utasema uongo?


Shahidi: Akiniambia niseme uongo nitasema ukweli ndiyo maana aliniambia niseme uongo nikakataa


Wakili: Ulichokisema 16/9/2021 ni uongo au ukweli ambacho unasema Wakili wako alikuambia useme?


Shahidi: Ulikuwa uongo


Wakili: Ule ulikuwa uongo


Shahidi: Ndiyo. Na huu ndiyo ukweli sasa


Wakili: Wakili ndiyo alikwambia useme uongo??


Shahidi:Ndiyo aliniambia kataa aliniambia ukikubali utafungwa


Wakili:Ni uongo gani umesema hapa mahakamani


Shahidi:Sijasema uongo wewe ndo unataka niseme uongo


Wakili:Nini kinakuzuia usiseme uongo leo?


Shahidi:Niko chini ya kiapo ndiyo kinanizuia nisiseme uongo


Wakili:Ni kweli wakati wa maelezo ya awali ulikataa kukutana na Mrosso


Shahidi:Kwa kifupi nilikataa vyote kwa maelekezo ya wakili


Wakili:Sasa bwana Watson 22/1/2021 wakati wewe unasema ulipelekwa pale kwa Mrosso na hilo kundi la watu la mshitakiwa wa kwanza ni kweli PW 13 hakuwa kati ya hao watu?


Shahidi:Sikuangalia watu hivyo siwezi kujua


Wakili:Ni kweli kwamba wakati wa ushahidi wake hapa mahakamani Ramadhan alisema hakuwepo kwa Mrosso na alipata kwa kupitia taarifa


Shahidi:Ndiyo


Wakili:Ni kweli siku hiyo umeeleza mahakama jana siku hiyo ulikuwa umefungwa pingu?


Shahidi:Nilifungwa pingu na kutolewa lock


Wakili:Ulifunguliwa pingu wakati gani?


Shahidi: Nilifunguliwa pingu ndani ya gari nikabebeshwa boksi lenye pump na kupeleka ofisini kwa Mrosso


Wakili: Ulifunguliwa pingu kwenye gari la nani


Shahidi: Gari la Sabaya VX


Wakili: Kama ulifunguliwa pingu ndani ya gari utakubaliana na mimi mtu aliyepo nje ya gari hawezi kukuona ukiwa na pingu? 


Shahidi: Ni sahihi


Wakili: Pw 13 Ramadhan alieleza mahakama kwamba wewe ulikuwa umefungwa pingu ukiwa kwa Mrosso.Je ulikuwa naye ndani ya gari?


Shahidi: Sikuwa naye ndani ya gari


Wakili: Wewe uliongea na Ramadhan kwa faraghà?


Shahidi: Haikuwa private kwa sababu askari alikuwepo


Wakili: Ramadhan alijuaje ulifungwa pingu?


Shahidi: Alisema kuna watu amefanya nao mahojiano ya awali na kupitia taarifa yeye ndo alipaswa aulizwe hilo swali


Wakili:Ulisikia ushahidi wa watuhumiwa wenzako wote wakisema 13 Ramadhan alienda gerezani akishawishi watuhumiwa hao waseme uongo kumkandamiza Sabaya kwa sababu wao wana nia ya kumfunga Sabaya na PW 13 aliwaambia mwenzenu mmoja ameshakubali kwamba yeye atasema uongo


Shahidi:Mimi sisemi uongo nasema ukweli.Niliwasikia wakisema hayo


Wakili:Ni kweli kwamba katika mashahidi wote wa jamhuri ambao walikuwepo kwa Mrosso kuanzia Mrosso,PW 4,PW 3 hakuna hata mmoja alisema alikuona umefungwa pingu?


Shahidi:Ni kweli


Wakili:Ni kweli wewe na Ramadhan mmepanga habari ya pingu ndiyo maana hata yeye  ambaye hakuwepo eneo la tukio ndiyo anazungumzia habari ya kufungwa pingu ili umkandamize Sabaya


Shahidi:Si kweli kabisa


Wakili:Ni kweli Rama atakuambia atakutoa kwenye kesi hii na atakupa Sh10 milioni 


Shahidi:Siyo kweli


Wakili: Unasema 20/1/2021 ulipeleka pump kwa Mrosso na ukasaini pale


Shahidi: Niliandika jina langu na namba za simu


Wakili:Hicho kitabu kipo?


Shahidi:Kipo 


Wakili:Ni sahihi kitabu hicho kingeletwa kingethibitisha wewe kuwepo 20/1/2021?


Shahidi: Angeulizwa Mrosso.


Wakili: Unataka kutuambia PW 13 mpelelezi bwana Rama alificha hicho kielelezo hakukileta hapa mahakamani


Shahidi: Mimi siwezi kujua


Wakili: Hivi kama hicho kitabu kipo kwanini PCCB au Mrosso hawakuleta


Shahidi: Mini sihusiki na PCCB na Mrosso wangeulizwa


Wakili:Kwanini hujakiomba kwa Mrosso ulete?


Shahidi:Nitaombaje kitabu wakati siyo cha kwangu


Wakili:Simu yako iko wapi?


Shahidi:Iko Takukuru


Wakili:Hujawahi kuwa na simu


Shahidi:Umesema wewe


Wakili:Tutajie Imeu namba ya simu yako


Shahidi:Sikumbuki na sitaki kuongea uongo niko chini ya kiapo


Wakili:Una risiti?


Shahidi:Nina risiti na boksi


Wakili:Hujawahi kuwa na simu


Shahidi:Ninayo


Wakili:Una kitambulisho cha taifa wewe


Shahidi: Ninayo 


Wakili: Huna 


Shahidi:Heeeee


Wakili: Namba ngapi kitambulisho chako?


Shahidi: Sikumbuki


Wakili: Simu yako ilichukuliwa na nani?


Shahidi: Shabani wa PCCB


Wakil: Una uthibitisho wa Shaban kuchukua simu yako,ulipewa risiti ya nakala ya ukamataji?


Shahidi: Mimi sina


Wakili: Mahakama itajiridhishaje simu yako ilikamatwa na Takukuru?


Shahidi:Itajiridhisha kwani shahidi Shaban alisema hapa mahakamani alikamata simu yangu


Wakili: Kwa nini hukuomba hiyo hati?


Shahidi: Ndiyo mara yangu ya kwanza na sikuwahi kujua mambo ya certificate


Wakili: Shaban alisema amekamata simu 10 alisema ni ya kwako?


Shahidi:Alisema amekamata simu zao zaidi ya 10 na mimi nikiwepo


Wakili:Ni watu wangapi walikamatwa Dar es Salaam?


Shahidi: Mimi, Sylvester, Sabaya, Enock, Saitabau na mke wa Sabaya


Wakili: Ulisema ile simu ina picha ya PW 4?


Shahidi: Sikusema simu yangu ina nini ndani


Wakili: Ulivyokua unaiomba ulitaka utuonyeshe nini?


Shahidi: Ingeletwa ningeonyesha


Wakili: Jana ulisema ulimpiga picha Mzee Kazibira na kumtumia Sabaya


Shahidi:Nilipiga ili kumthibitishia Sabaya aikuwa mtaani alipokuwa anasema


Wakili: Picha iko kwenye simu yako?


Shahidi: Ndiyo iko kwenye simu yangu kwenye meseji za whatsapp


Wakili:Unataka kusema PCCB hawajui kufanya uchunguzi,wakamate simu yenye picha wasiilete mahakamani?


Shahidi:Mimi sijawahi kufanya kazi PCCB


Wakili:Baada ya kumaliza darasa la saba ulienda kozi ya kutambua sauti ya mtu kwenye electronic device?


Shahidi:Hapana


Wakili:Mtu wa darasa la saba anawezaje kujua sauti ya mtu kwenye simu?


Shahidi:Hata mtoto anajua sauti ya baba yake kwenye simu


Wakili: Ni baba yako?


Shahidi:Hapana ila sauti ya Sabaya naijua nikiwa naongea naye


Wakili: Sasa ni kweli kwamba jana ulieleza mahakama kwa muda huu hakuwahi kukupigia simu kwa simu yake?


Shahidi: Nilichoeleza ni vinavyohusiana na kesi. Amewahi kabla kunipigia ila niliyoeleza jana hakuwahi kunipigia kwa simu yake


Wakili: Unasema ulikuwa unampiga picha Sabaya alikuwa anakulipa?


Shahidi:Ndiyo


Wakili:Ulikuwa unampa risiti


Shahidi:Sina kitabu cha risiti wala Tin namba


Wakili:Umesema umewahi kumpiga picha Sabaya akiwa na Askofu Masangwa na Mchungaji Mollel


Shahidi:Ni kweli


Wakili:Ziko wapi?


Shahidi:Yeye ndo anazo nilimkabidhi Mile Stone


Wakili:Ni kweli kwamba zile picha ukipiga unaziweka kwenye laptop unatèngeneza unachukua USB unampa?


Shahidi:Ndiyo


Wakili:Ulikuwa unatumia nini?


Shahidi: Kamera Canon 7D Mark two


Wakili: Hiyo kamera na laptop ziko wapi


Shahidi: Kamera niliuza nikanunua nyingine lakini laptop ipo


Wakili: Kwanini hukuleta laptop?


Shahidi: Storage ilikua inajaa unafuta picha za mteja


Wakili: Nitakuwa sahihi nikisema ile laptop haina picha za Sabaya


Shahidi: Inazo nyingi


Wakili: Kwa nini hukuleta laptop wakati ingethibitisha ulikuwa mpiga picha wa Sabaya?


Shahidi: Kwa sababu nilitaka kuleta simu


Wakili: Unajua effect ya maneno yako? Unataka kufunga mwenzako miaka 20 kwanini hujaleta laptop


Shahidi: Sina nia ya kumfunga na laptop ninayo


Wakili: Wewe hujawahi kuwa mpiga picha wa Sabaya


Shahidi: Nilikuwa mpiga picha wake na hata video za YouTube kuna baadhi ya picha ninaonekana nikiwa na kamera


Wakili:Wewe unajua sauti ya Sylvester?


Shahidi:Ndiyo


Wakili:Unajua nchi hii kuna watu wana ajira wanaiga sauti za viongozi


Shahidi:Najua


Wakili:Kwanini  ulienda kumuibia Mrosso


Shahidi:Sikumuibia 


Wakili:Unafahamu kilicholeta matatizo yote ni Pump ambayo haikupewa risiti ya kielektroniki na usingepeleka pump watu wako wa kundi lako la mtu mwenye benzi msingemuibia Mrosso Sh90 milioni


Shahidi:Siyo kweli


Wakili:Uliwahi kuwaeleza PCCB ulikuwa na sabaya na dereva wa serikali anaitwa Kivuyo na mkaenda kwa Mrosso


Shahidi: Hapana


Wakili:Kwa hiyo umekuja kueleza baada ya Rama kukutengeneza gerezani?


Shahidi:Rama hakunitengeneza kwa chochote na hayo mambo ya kumkandamiza mtu nasikia kwako


Wakili:Unasema uliitwa Point Zone


Shahidi:Ndiyo


Wakili:Hukueleza kumuona mtu yoyote zaisi ya sabaya kati ya hawa washitakiwa wengine


Shahidi:Ni kweli nilieleza


Wakili:Hukuwaeleza kwa sababu hawakuwep


Shahidi:Sikuwaona niliona walioshuka kwenye gari


Wakili:Uliwahi kushiriki kikao chochote Point Zone 


Shahidi:Sikuwahi kushiriki nimesema nilikuta magari yanatoka


Wakili:Jana ulisema mbele ya mahakama sabaya ni mtu wa hatari


Shahidi:Ni kweli


Wakili: Ulijua Sabaya ni mtu hatari lini?


Shahidi: Nilijua Sabaya ni mtu hatari 2020


Wakili: Sabaya alikupiga sana


Shahidi: Ndiyo akishirikiana na walinzi wake


Wakili: Kwa hiyo unatamani afungwe


Shahidi: Roho yangu haiko hivyo


Wakili: Unatamani aachiwe?


Shahidi:Mahakama ndiyo itaamua siwezi kuipangia


Wakili:Umesema wewe umeishi na Sabaya kama mateka?


Shahidi:Ni kweli


Wakili:Wewe unasema Sabaya amekuwa akikupiga, kukiweka lock up na matendo ya kukuumiza hivi hayo matendo ni kabla ya 20/1/2021


Shahidi:Ni kabla na baada


Wakili: Pamoja na yote hayo uliendelea bado kupokea simu zake?


Shahidi:Ndiyo maana nikasema nilikuwa mateka


Wakili: Ulisema ulilalamika kwenye vyombo vya dola lakini haikusaidia


Shahidi: Ndiyo


Wakili: Uliripoti wapi?


Shahidi:Niliripoti kwa RCO kwa bwana anaitwa Mushi na usalama wa taifa


Wakili:Wewe unashangaza sana wakati Sabaya anatoa ushahidi ulimuuliza maswali hayo na kukupiga?


Shahidi:Wakati anatoa ushahidi nilikuwa na wakili 


Wakili:Kwanini hukumkataa


Shahidi:Kwa sababu sikutaka kufanya anachotaka kufanya yeye


Wakili: Kwa nini hukuwahi kuwaambia washitakiwa wenzako unawajua


Shahidi: Wakili asingetaka na kuna maswali nilikuwa nampa kwa mashahidi hapa lakini alikuwa haulizi na hata akija gerezani alikuwa anawasiliana na Sabaya. Wakili wangu mteja wake alikuwa Sabaya, hakuwa anaongea na mimi


Wakili: Kwanini hukumuuliza Enock mnafahamiana, mlikamatwa wote 


Shahidi: Sikumuuliza maswali kwani sikuwa na mwelekeo wa maswali ya kuuliza


Wakili: Sasa mtu hatari kama Sabaya kwanini akutume wewe kupeleka pump?Jana ulisema alikutuma upeleke pump au kuna mzigo umpokelee?


Shahidi:Aliniambia mwenye namba hiyo anakuja na mzigo


Wakili:Je Sabaya alisema ni mzìgo gani?


Shahidi:Hakusema kabisa


Wakili:Je ni kweli kulingana na ushahidi wako aliyekuonyesha gereji ni Sabaya?


Shahidi: Aliyekuja na benzi nyeusi akitokea Bomang"ombe


Wakili:Ni kweli Sabaya hajawahi kukutumia pesa ya kulipa pump


Shahidi:Hajanitumia


Wakili:Ulienda kutengeneza pump kwa maagizo ya mwenye?


Shahidi:Kwa maelekezo ya Sabaya


Wakili:Ni kweli kwamba Sabaya aliwahi kuunda genge na wewe


Shahidi:Sijawahi kuunda genge lolote na Sabaya


Wakili:Ni kweli Sabaya, Enock waliunda genge na wewe mkaenda kwa Mrosso na kuchukua rushwa ya Milioni 90


Shahidi:Sijui mimi niliondoka pale kwa kutoroka


Wakili:Mtu anayetoroka anaweza kumfata anayemtoroka hadi Dar umbali wa kilomita 600, mtu hatari ukafika ukala chakula chake


Shahidi: Ndiyo maana niliekeza nilikuwa mateka na nilieleza sikumfata Sabaya Dar es Salaam,nilimfuata mjomba wangu 


Wakili: Hivi ni kweli ulisema sabaya alikwambia maeneo hayo ni hatari


Shahidi:Niliaga naondoka akaniambia ni usiku sana siyo kuzuri kwa hiyo nipumzike nitaondoka asubuhi


Wakili:Mtu anayekutesa anaweza kuwa concerned na security yako?


Shahidi:Alifanya hivyo kwa sababu nilichukua mzigo wake na kumpelekea Dar

HABARI HIZI ZINAPATIKANA  KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO BURE

________________________________

 Join AJIRA YAKO Group for Daily Job Updates CLICK HERE


Post a Comment

0 Comments