Risasi iliyomuua Mwanakijiji Mgodini inavyozua Mtafaruku

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA



"TULIMKUTA akiwa ameanguka chini, amepigwa risasi paja la kulia, ikatokea upande wa pili. Hata 'kulwa na doto' (sehemu za faragha) walikuwa wamebomolewa vibaya," Yunge Sheka, mkazi wa Kitongoji cha Mwamala, Kijiji cha Igumangobo wilayani Kishapu, anakumbuka mkasa uliojaa simanzi na chanzo-

Baba mzazi wa marehemu Cosmas, Hamis Kushilimwa (wa pili kulia), akifanya mahojiano na Ofisa Mipango Mwandamizi wa LHRC, Wakili Joyce Komanya, kijijini Igumangobo wilayani Kishapu hivi karibuni. PICHA: MPIGAPICHA WETU
- cha kifo cha mtoto wake wa kwanza.

Yunge (48), akiwa ameketi kwenye gogo nje ya nyumba yake, mwili wake akiutanda kwa khanga, anaendelea kusimulia kuwa ilikuwa Machi 10, mwaka huu kijiji hicho kilipotawaliwa na simanzi pale kijana wao, Cosmas Hamis (23), alipofariki dunia kwa kupigwa risasi jirani na mgodi wa almasi wa El Hilali, mahali ambako siyo mbali na alikokuwa anaishi.

Hapo ni umbali wa Km 23.6 kaskazini mashariki mwa Mji wa Shinyanga na safari yake kwa gari kutoka mjini Shinyanga inachukua takriban nusu saa ukifuata barabara ya lami ya Shinyanga-Mwanza kisha unachepuka kulia kuifuata barabara ya vumbi kupitia Utemini, kijiji maarufu kwa watafutaji wa almasi nchini.

Yunge anasema ni mkasa ulioibua taharuki na mvurugano, akisimulia kwamba siku hiyo mwanawe Cosmas waliyekuwa wanaishi naye, aliwafuata shambani saa tatu asubuhi, akiwaaga anakwenda kutafuta riziki.

Mama huyo anaendelea kuwasilisha kilichojiri kwamba, wakiwa wamesharejea nyumbani, wakapata taarifa mtoto wao amepigwa risasi na amedhurika vibaya katika eneo jirani na mgodi huo.


Yunge anasema ni taarifa zilizowafanya wachukue uamuzi wa haraka kuelekea eneo la tukio, ambako siyo mbali na wakaushuhudia ukweli huo.

Anasema kuwa mara moja, baba wa marehemu kwa kushirikiana na wanaume wenzake, walichukua gari kumwahisha kwenda Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya matibabu.

Mama huyo anayezungumza kwa sauti ya chini, inafika hatua simanzi inamtawala, anasita kuendelea na ufafanuzi wake, akihamia kwenye kilio.


Wakati Nipashe ikiendelea kudadisi, baba wa marehemu, Hamis Kushilimwa (50), analazimika kuendeleza mazungumzo hayo, akifafanua kwamba wakiwa njiani kuelekea hospitalini, mwanawe akawa anaendelea kutokwa na damu nyingi na hatimaye umauti ukamkuta umbali si mrefu na wote wakaridhiana kuurejesha mwili eneo la tukio.

Anasimulia kwamba baada ya kurudi eneo la tukio, waliushusha mwili na kupiga mbiu ya kimila, iliyokusanya umma wa kijijini ukiongozwa na askari wa sungusungu waliozonga eneo hilo, wengi wakiwa na hisia za 'hatukubali'.

Kwa mujibu wa mzazi huyo, ni hali ya mshikemshike iliyotawala mahali hapo na kijiji kizima, ujumbe ukifika ng'ambo kutoka waliko mgodini na ilipotimu saa saba usiku, polisi waliwasili na gari lao wakiwa na diwani na mwenyekiti wa kijiji, wakaomba wananchi wawe watulivu, hata wakapewa mwili kwa ajili ya uchunguzi hospitalini.

Kushilimwa ananukuu mrejesho wa kwanza waliopewa hospitalini kwamba uchunguzi ulifanywa Machi 11 na kilichogundulika mwanawe alipigwa risasi katika namna aliyoieleza mama yake na siku iliyofuata Machi 12 walikabidhiwa mwili.


Hapo ndipo baba huyo anasema ukaibuka utata wenye sura mbili. Mosi; hata kabla ya kuupokea mwili huo, hawakuwa tayari kuuchukua kwani kiuchumi walikuwa hoi, hawana pesa za kuusafirisha kutokana na hali yao duni, huku mtegemezi wao ndiye aliyetangulia mbele ya haki.

Pia ufafanuzi wa kisheria waliopewa kutoka kwa Ofisi ya Upelelezi ya Polisi Mkoa wa Shinyanga, ulibainisha Cosmas aliuawa na polisi waliotumia bunduki aina ya 'Sub Machine Gun', maarufu SMG.

Kwa mujibu wa baba wa Cosmas, ufafanuzi huo ulimwekea utata kwenye uelewa wake kwani kwa hatua zote za awali na ilivyoeleweka hata kijijini kwake Igumangobo, kitendo hicho kilifanywa na askari wa mgodini.

Anasema kutokana na sintofahamu ya kipato, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO) ambaye hakumtaja jina, aliwakabidhi Sh. 100,000 kwa ajili ya kukodi gari la kuusafirisha mwili, tayari kwa maziko kijijini.


"Mwili ulipofikishwa hapa nyumbani, ulizikwa na umati mkuwa wa watu ukizingatia askari wa sungusungu nao walikusanyika hapa kutokana na kifo cha mwanangu kuwa cha uonevu," Kushilimwa anasema.


Kibali cha kuzika mwili wa Cosmas Hamis kilichotolewa na Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga.
MWENYEKITI WA KIJIJI

Abeid Jilala, Mwenyekiti wa Kijiji cha Igumangobo kilichoko Kata ya Idukilo, ana ufafanuzi zaidi kuhusu tukio la mauaji ya kijana huyo na hatua zilizochukuliwa, akitamka:

"Cosmas alipigwa risasi akiwa karibu na eneo la machimbo ya almasi katika Kijiji cha Mwanholo, Kata ya Lohumbo. Tulimkuta damu inamwagika kama maji.

"Polisi walifika saa 7:14 usiku, kabla hawajafika eneo la tukio, wananchi waliambiwa wapungue, waende majumbani maana wengi wao walikuwa wamekasirishwa na mauaji hayo. Kilichofuata sisi viongozi tuliwaachia polisi wafanye uchunguzi ili serikali ichukue hatua stahiki.

"Licha ya tukio hilo, bado wananchi wanaendelea kwenda kuchimba. Mvua mwaka huu imegoma, tegemeo pekee la kipato kwa sasa hapa ni uchimbaji wa madini.


"Vijiji vinavyowika sana kwa kutoa mawe (almasi) ni Mwanholo na Nyenze. Wachimbaji wanatoka vijiji jirani na maeneo haya vya Ikudiko, Utemini, Buganika, Maganzo, Masagala, Wizunza, Buchambi na hata Kolandoto."   

KAULI YA MGODI

Antony Rafael, Kaimu Meneja wa Mgodi wa El Hilali, katika mazungumzo na Nipashe, anakiri askari polisi waliokuwa wanalinda mgodi wao, walihusika katika mauaji ya kijana Cosmas.

"Kilichotokea ni kwamba waliingia hapa mgodini kwa kutuvamia, walikuwa wengi, zaidi ya 20. Wengi walikimbia baada ya polisi kufyatua risasi hewani, walibaki watatu wakawa wanapambana na polisi.

"Kuna mmoja wa askari aliyejeruhiwa, katika kujihami ndipo akampiga risasi huyo aliyefariki dunia (Cosmas). Ndicho kilichotokea, hakuna tukio lingine zaidi kwa sasa tangu lilipotokea hilo (la mauaji ya Cosmas)," Rafael anasema.

Nipashe inapohoji uhalali wa askari walinzi wa mgodi kuua watu kwa kuwapiga risasi, Rafael ana ufafanuzi, akitamka: "Hao ni wavamizi. Mtu amekuvamia, lazima ujihami. Sasa katika huko kujihami, ndicho hicho kilichotokea."

HOSPITALINI SHINYANGA

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga, Dk. Luzila Boshi, katika ufafanuzi wake kwa Nipashe kuhusu kifo cha Cosmas, anakiri hospitali hiyo kuufanyia uchunguzi mwili wa kijana huyo.

"Ni kweli tuliupokea mwili wa Cosmas Machi 11, mwaka huu na wataalamu wetu hapa waliufanyia 'postmortem' (uchunguzi). Mwili uliletwa hapa hospitalini na polisi ili ufanyiwe uchunguzi, ulikabidhiwa kwa ndugu Machi 12, mwaka huu.

"Yule mtu (Cosmas) alikuwa anasadikiwa kupigwa risasi, na ni kweli alikuwa amepigwa risasi kwenye mguu. Sisi tulifanya postmortem na matokeo ya postmortem tuliwakabidhi polisi. Kwa mujibu wa taratibu za kisheria, wao (polisi) ndiyo wenye mamlaka ya kutangaza kilichobainika kwenye postmortem," anafafanua.

Kwa mujibu wa kibali cha kuzika mwili wa Cosmas kilichotolewa na Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga Machi 11 mwaka huu, chanzo cha kifo cha kijana huyo kimetajwa kwa lugha ya kitabu kwamba ni ‘Hypovolemic shock secondary to penetrative wound’.

Kwa tafsiri isiyo rasmi, ni kupungua kwa damu mwilini kutokana na jeraha lililosababishwa na kuchomwa na kitu chenye ncha kali.

-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad