Alichozungumza Freeman Mbowe na Watanzania Waishio nje ya Nchi (Diaspora)

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

 


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema Watanzania wanahitaji katiba mpya ambayo itatengeneza mfumo bora wa utawala wa nchi badala ya kuacha kila uamuzi kufanywa na Rais.


Mbowe aliyasema hayo jana Jumamosi Juni 4, 2022 wakati akizungumza na Watanzania waishio nje ya nchi (diaspora) kwa njia ya teknolojia akiwaeleza masuala mbalimbali ya kitaifa pamoja na mipango ya chama chake.


Alisema Chadema kina mpango mzuri wa kurudisha madaraka kwa wananchi na kuondoa mifumo yote inayoelekeza mamlaka kwa watu wachache au mtu mmoja kuamua juu ya maisha ya Watanzania zaidi ya milioni 60.


“Sisi Chadema tunahitaji ku-decentralize (ugatuzi), nchi nyingi wamefanya hivyo. Tanzania tunaweza tukaanzisha kanda 10 kama za Chadema na zikawa zone na Serikali yake na Bunge lao dogo linalojitegemea na kujipangia sheria zao.


“Kwa hiyo lazima twende kwenye kanda au majimbo…wanakuwa na magavana wao na wanachaguliwa na wananchi, sio watu wa kuteuliwa. Unateua mtu ambaye hana attachment yoyote na wale watu anakwenda kuwaongoza, hilo linatakiwa kukomeshwa,” alisema.


Alisisitiza kwamba hakuna mkoa ulio masikini hapa nchini, kwa sababu kila mkoa una utajiri wa rasilimali zake, hata ile mikoa iliyotambulika kuwa masikini kama Mtwara na Lindi, ina utajiri mkubwa.


ADVERTISEMENT

“Lazima tu-address wapi tunapokwama mambo ya msingi, tunajikwamuaje kwa kuiangalia katiba, mifumo yetu ya utawala, utawala uwe kwa watu, watu waamue viongozi wao, wawachague viongozi wao.


“Katiba ihakikishe kwamba tunajenga taasisi imara, mabunge katika kanda ambayo yanawajibika, mabunge yatakayoangalia maslahi ya wananchi. Tunahitaji mahakama ambayo ni huru. Lazima tuwe na katiba ambayo itaweka makatazo,”alisema Mbowe.




Suala la elimu




Mbowe alisema Tanzania inahitaji kufumua mfumo mzima wa elimu kwa sababu watu wengi bado wamelemaa na mfumo wa vyeti, ndiyo maana kumekuwa na wizi wa mitihani shuleni na vyuoni.


“Wakishaingia Wakenya, Wazimbabwe na Waganda, tunapoteza. Zinakuja multinational companies zinalazimika kuajiri watu kutoka Afrika Kusini lakini wanashindwa kuwachukua vijana kutoka Dar es Salaam licha ya kwamba ni nafuu kwa maana ya gharama za uendeshaji,” alisema.


Alisisitiza kwamba Kiswahili ni kizuri kutumika lakini kisiitoe Tanzania katika ulimwengu wa ushindani ambao nayo iko ndani yake. Alisisitiza kwamba kama Tanzania haiwezi kushindana katika mchangamano na mataifa mengine basi hakuna manufaa yoyote.


“Unakuta hawa watunga sera wetu wanakwambia tufundishe Kiswahili kuanzia chekechea mpaka chuo kikuu, sawa, lakini ni watu hao hao ambao wanawapeleka watoto wao katika shule za English Medium.


“Wanawapeleka watoto wao kusoma Afrika Kusini, China, Uingereza, ili mradi wapate ile exposure. Hata wakisoma ndani ya nchi, wanasoma katika shule ambazo ni za English Medium,” alisema Mbowe.


Alisema watoto ambao wanasoma kwa lugha za kigeni kama Kiingereza wanafanya vizuri hata katika soko la ajira, ndiyo maana ukienda mataifa ya Dubai utawakuta Wakenya wengi au raia wa Afrika Kusini.




Hoja ya maridhiano




Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema maridhiano imekuwa ni sehemu ya uendeshaji wa chama hicho kwa miaka mingi lakini Serikali ya awamu ya tano haikutaka maridhiano kwa sababu iliamini upinzani ni tishio.


Alisema baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani, Chadema walikuwa na shauku ya kuzungumza naye, walimwandikia barua ya kuzungumza naye wakiamini kwamba wanahitaji kuwa na maridhiano.


Mbowe alisema hata alipotoka gerezani baada ya kuachiwa, hakusita kupokea wito wa Rais Samia alipomtaka kwenda kuzungumza naye Ikulu. Alisema anaona dhamira njema katika majadiliano ambayo wamekuwa wakifanya baina ya chama chake na CCM.




“Niseme wazi kwamba hadi wakati huu nimeona dhamira njema ya Rais Samia katika mazungumzo ambayo tumeyafanya na tutaendelea na mazungumzo hayo kwa awamu tofauti. Kama dhamira hiyo itaondoka basi hatutasita kujiondoa kwenye mazungumzo hayo,” alisema.


Mwanasiasa huyo mkongwe aliwataka wanachama wa Chadema kuwa wavumilivu wakati majadiliano hayo yanaendelea huku akiwahakikishia kwamba kila kitu kitakwenda vizuri kwa maslahi ya chama chao.




Mgogoro NCCR Mageuzi




Akizungumzia mgogoro ndani ya NCCR Mageuzi, Mbowe amesema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imekuwa ikiingilia masuala ya ndani ya vyama vya siasa na kusababisha mgogoro ambayo inadhoofisha vyama.


Aliitaka ofisi hiyo isiingilie masuala ya uendeshaji wa vyama nchini bali ivilee na kuvisimamia bila kuviingilia na kusababisha mifoforo ndani yake kama ilivyotokea hivi karibuni ndani ya NCCR Mageuzi.




Wadau wengine




Akichangia kwenye mjadala huo, mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Azavery Lwaitama alisema amefurahishwa na suala la ugatuzi wa mamlaka ya dola ambao siyo kwa Tanzania Bara na Zanzibar bali kuigawa Tanzania katika kanda zake.


Alisema anakubaliana na hoja ya Mbowe kwamba Chadema ni chama cha wote, wajamaa na wasio wajamaa, hivyo, ni muhimu kuvumiliana katika kufanya siasa ndani ya nchi.


“Chama kilianzishwa na mtu aliyekuwa anabishana na Nyerere lakini mzalendo na Mwalimu Nyerere alikubali kuwa ni mzalendo.


Umeliweka vizuri kwamba Chadema ni chama cha wote na kila mtu ana haki ya kuwa mwanachama wa Chadema bila kujali ni mjamaa au siyo mjamaa, alisema Dk Lwaitama wakati akichangia kwenye mjadala huo.

-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad