Ticker

6/recent/ticker-posts

Simulizi ya Mtaka kuhamishwa hamishwa

Mikoani. Mkuu wa Mkoa mteule wa Njombe, Anthony Mtaka amesimulia siri ya kupelekwa kwenye mikoa iliyo nyuma kimaendeleo huku akieleza deni aliloliacha Dodoma.

Mtaka alisema hayo jana, baada ya kuulizwa maoni kuhusu uteuzi wake mpya wa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe akitokea Dodoma alikokaa kwa takribani siku 440, akitoa Mkoa wa Simiyu.

Juzi usiku, Rais Samia Suluhu Hassan alifanya uteuzi wa wakuu wa mikoa wapya, wengine kuachwa na kadhaa kuhamishwa vituo vya kazi, akiwamo Mtaka anayetoka Dodoma na kuhamia Njombe.

Alisema Rais ndiye mwenye jukumu la kuteua, hivyo yeye anashukuru popote atakapopangiwa kwenda kufanya kazi.


 
“Mimi kama kijana namshukuru Rais kwa kuendelea kuniamini, kwangu naichukulia kama heshima kubwa kwa dhati ya moyo wangu. Namshukuru sana chini ya miaka 40 marais watatu kukuamini ni jambo kubwa, namwambia asante sana,” alisema Mtaka.

Alisema siku zote katika maisha yake ni muumini wa kufanya kazi na si kituo cha kufanyia kazi na kazi anazofanya kama Mkuu wa Mkoa ni zile zinazohusu wananchi na kuhakikisha maisha yao yanaboreka.

Mtaka, aliyewahi kuwa Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) alisema Mkoa wa Njombe una fursa nyingi, hivyo atahakikisha katika sekta ya elimu mkoa unaongoza katika matokeo ya darasa la saba, kidato cha nne na hata cha sita.


Alisema kutokana na mkoa huo kuwa na hali ya hewa nzuri kwa kilimo, atasimamia uuzaji wa maua nje ya nchi.

“Kingine hali ya hewa ya Njombe inaruhusu ukuaji wa uchumi wa wananchi, nitahakikisha nawasaidia vijana kutimiza ndoto zao wanazotaka kuzifikia,” alisema Mtaka, ambaye enzi za utawala wa Rais John Magufuli alimsifia kama mkuu wa mkoa bora.

Kuhusu mradi wa Liganga na Mchuchuma, Mtaka alisema umezungumzwa muda mrefu, hivyo sasa ni wakati wa kuufanya kwa vitendo.

Mtaka alisema licha ya kuhamishwa kituo cha kazi Dodoma, ameacha mradi wa kielelezo wa soko la wamachinga ambapo anadai ametekeleza kwa vitendo maagizo ya Rais Samia.


 
“Simiyu niliacha kiwanda kikubwa cha chaki, Dodoma nimeacha project kubwa ya wamachinga na ikikamilika itakuwa ni suluhisho na kielelezo kikubwa kama mkoa tumetoa taswira mapato ya ndani yanavyoweza kufanya vizuri,” alisema Mtaka.

Pia, alisema amefungua fursa kwa vijana wa bobaboda, kwani wameweza kujiongezea kipato pamoja na kujiajiri.

“Naamini kwa mwaka mmoja upo mchango wangu, hasa kuchangia kipato chao. Nimejenga timu naondoka Dodoma nikiwa nimeacha familia moja, nimefanya kazi vizuri na makundi ya sekta binafsi pamoja na kuuheshimisha utumishi wa uuma,” alisema Mtaka.

Kauli ya Mchungaji Msigwa

Mbunge wa zamani wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alisema angetamani kuona Mkuu wa Mkoa aliyehamishiwa Rukwa, Queen Sendiga anabaki Iringa.


“Ningependa Sendiga abaki Iringa kwa sababu alikuwa anaenda vizuri, alikuwa ni kiongozi anayewaunganisha watu na aliwaheshimu wote,” alisema Mchungaji Msigwa.

Sendika katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 alikuwa mgombea urais kupitia ADC na Rais Samia aliwahi kueleza Serikali anayoingoza itashirikiana na kila mmoja bila kujali itikadi ya chama chake.

Kuhusu Halima Dendego anayekwenda kuwa mkuu wa mkoa Iringa, Mchungaji Msigwa alisema kwa sababu hajawahi kufanya naye kazi itakuwa vigumu kumwelezea.

Halima amewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, kisha kuwekwa kando la Rais Magufuli.

Naye Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Iringa, Hilary Kipingi alisema kwa muda mfupi waliofanya kazi na Sendiga, alionyesha weledi bila kujali nafasi yake au kama mtu ambaye siku moja atahamishiwa mkoa mwingine.


 
Kagaigai ashtua

Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro walisema kuondolewa kwa Steven Kagaigai kuwa mkuu wa mkoa huo kumewashtua kwa kuwa ni kati ya viongozi waliokuwa wachapa kazi na aliyejipambanua kama ni mtu wa haki na aliyepambana kuuinua mkoa katika sekta za elimu, utalii na mazingira.

Hata hivyo, wananchi hao wamesema pamoja na mazuri mengi ya uongozi wake, ziko changamoto ambazo mrithi wake, Nurdin Babu ambaye alikuwa mkuu wa wilaya ya Longido, Arusha anapaswa kuzifanyia kazi.

Baadhi ni suala la migogoro kati ya wakulima na wafugaji huko Siha na Wilaya ya Same inayotokana na baadhi ya wakulima kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima.

Changamoto nyingine ni wimbi la wizi wa miundombinu ya taa za barabarani katika mji wa Moshi ambapo katika kipindi kifupi, taa za sola na betri zake zimeibwa kwa karibu asilimia 60 katika barabara za Tembo, Sukari na inayoelekea kiwanda cha Bonite na haijulikani soko la taa hizo ni wapi na nani hasa wanaokula njama na kuiba betri na paneli za sola.

Mbali na changamoto hiyo, pia mrithi wa Kagaigai anakabiliwa na changamoto ya kukithiri kwa biashara ya mirungi inayoingizwa nchini kutoka Kenya kupitia njia za panya pamoja na biashara ya wahamiaji haramu kutoka Somalia na Ethiopia waliofanya mkoa wa Kilimanjaro kama moja ya lango la kuingia nchini kuelekea Afrika Kusini na baadaye nchi za Ulaya.

Akizungumza na Mwananchi jana, Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema alisema hafahamu sababu za kuachwa kwa Kagaigai, lakini akasema huo ni uamuzi wa Rais ambao amepewa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.

Kwa upande wake, Charles Mboya, mkazi wa Bomambuzi, alisema ni vigumu kufahamu kwa nini Kagaigai ameachwa, lakini ameondoka akiacha changamoto ambazo mrithi wake anapaswa kukabiliana nazo ambazo ni pamoja na wamachinga kurejea mitaani na suala la wizi wa taa za barabarani ndani ya mji wa Moshi ambalo linafanywa na watu wasiojulikana.

Mgogoro katika Jiji la Arusha ambao unatokana na tuhuma za ubadhirifu wa fedha uliibuliwa na Mbunge wa Arusha (CCM) Mrisho Gambo katika mkutano wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kusababisha kuondolewa Mkurugenzi wa Jiji, Dk John Pima.

Pima na maofisa wa idara ya fedha tayari wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za ubadhirifu na utakatishaji wa fedha.

Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alisema mbunge kuibua tuhuma za ubadhirifu wa halmashauri ilikuwa ni dosari kwa Katibu Tawala wa Mkoa.

Mkoani Morogoro baadhi ya wananchi wameeleza kuwa watamkumbuka Martine Shigela kwa namna alivyopunguza kwa asilimia 80 migogoro ya wakulima na wafugaji iliyokuwa kero, hasa kwenye Wilaya za Kilosa, Mvomero, Morogoro (DC), Ulanga na Kilombero, huku wakimtaka Fatuma Mwasa kufuata nyayo za Shigella katika kutatua kero hiyo kubwa. Shigela amehamishiwa Mkoa wa Geita.

Aidha, wananchi hao walisema watamkumbuka kwa namna alivyoratibu na kusimamia wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga na pia ujenzi wa madarasa kwa fedha za Uviko-19.

Nickolaus Mshana, mkazi wa Misongeni Bigwa alisema Shigela ni mmoja wa wakuu wa mikoa walioonyesha kuuweka mkoa katika hali ya utulivu, ikiwa ni pamoja na kupunguza kwa kiasi kikubwa migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo awali ilisababisha kukosekana kwa amani kwenye maeneo yenye migogoro.

Mkoani Tanga, ni takriban mwaka mmoja na miezi miwili ya utumishi wa Adam Malima akihudumu katika mkoa hiyo, kisha kuhamishiwa Mwanza.

Malima, ambaye aliripoti Mei mwaka 2021, ameacha alama ya kuwahamasisha viongozi na watendaji waliokuwa chini yake kuhakikisha kila mmoja anatumia nafasi yake kuwatumikia wananchi katika sekta ya kilimo, hususan cha mkonge, mazao ya chakula, ufugaji na uvuvi wenye tija.

Aidha, Malima pia ameacha alama katika michezo baada ya kuinusuru timu ya Coastal Union kushuka daraja msimu uliopita na kuiwezesha kucheza fainali na Yanga kombe la Azam.

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Tanga, Hamad Kidege alisema Malima alitumia kipaji chake katika kuhamasisha shughuli za kuuinua kiuchumi mkoa wa Tanga katika sekta ya utalii, mazingira, kilimo, uvuvi na ufugaji.

Imeandikwa na Ramadhan Hassan (Dodoma), Janeth Joseph (Kilimanjaro), Tumain Msowoya (Iringa), Mussa Juma (Arusha), Lilian Lucas (Morogoro) na Burhani Yakub (Tanga).

Nafasi za Ajira Jiunge na Ajira Yako Telegram Group

 CLICK HERE


Post a Comment

0 Comments