UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Nani anastahili kuwa mchezaji bora wa msimu?

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA




USIKU wa leo pale Rotana Hotel ndipo mijadala itakapoanzia tuzo za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zitakapotolewa.

Haitokei Tanzania tu bali Dunia nzima, tuzo huwagawa wadau katika makundi tofauti ya mitazamo. Zipo tuzo zisizokuwa na mijadala kama ile ya mfungaji bora lakini nyingine nyingi hubaki kuwa ni maoni ya wahusika.

Nimekuwa nikisema mara nyingi linapokuja suala la ubora linabaki kuwa ni suala la maoni binafsi.

Kila mmoja ana haki ya kuweka vigezo vyake na kuchagua anachoamini kwake yeye ni bora. Huwezi kumpinga kwa sababu hakuna kigezo chochote duniani cha kupima ubora wa binadamu. Tunaweza kupima ubora wa bidhaa lakini si binadamu.


 
Hivyo na mimi nitasema kuhusu mtazamo wangu katika kipengele kimoja ambacho nafikiri kitawaacha mashabiki katika makundi tofauti. Tuanzie hapa kwa mchezaji bora. Tabu imeanzia alipokosekana jina la mshambuliaji kiongozi wa Geita Gold, George Mpole ambaye anaweza akavaa jezi ya Simba msimu ujao. Kwamba Mpole hakuwa katika wachezaji watatu bora wa msimu?

Kwamba Henock Inonga alifanya vyema kwa Simba kuliko Mpole alivyofanya kwa Geita msimu mzima? Nafikiri hapa kamati ya tuzo walipepesa macho na kuamua kuweka mzani sawa kati ya Simba na Yanga.

Jina la Mpole lilipaswa kuwepo kati ya wachezaji wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa msimu. Si kwa sababu ya kuibuka mfungaji bora lakini nafikiri tukitafuta wachezaji watatu waliozisaidia zaidi timu zao, nadhani huwezi kulikata jina la Mpole.


Kwa hiyo kati ya hawa watatu nani anastahili? Kwanza nafikiri Inonga si mshindani hapa. Kama tu nadhani Mpole alipaswa kufikiriwa badala yake, vipi nikubali yeye kutwaa tuzo ya mchezaji bora? Nafikiri ataibuka mshindi wa tatu.

Shida ni kufanya maamuzi kati ya wale mashujaa wawili wa Yanga, Yanick Bangala na Fiston Mayele. Kumchagua mmoja wao ni kazi iliyojaa ukatili na lawama ukizingatia vitu ambavyo wamefanya kwa klabu yao.

Mabao ya Mayele yameisaidia Yanga kutwaa ubingwa. Zipo pointi ambazo Yanga wangezidondosha kama isingekuwa Mayele. Yapo mabao ambayo Mayele alifunga kwa jitihada binafsi na kuwatoa Yanga katika mdomo wa mamba.

Lakini kuna nyakati wale viungo na washambuliaji wa Yanga walifunga kwa sababu ya uwepo wa Mayele uwanjani. Mabeki walipokuwa bize kupambana nae, wengine walipata nafasi ya kufunga. Ni sababu hizo zinawafanya wengi waamini Mayele anastahili kuwa mchezaji bora wa msimu.


 
Lakini vipi kuhusu Bangala? Nilisema mahala fulani, Bangala anastahili kuwa mchezaji bora wa msimu. Hata hapa sitabadilisha mtazamo wangu! Inawezekana mabao ya Mayele yameipa Yanga pointi tatu katika viwanja vingi sawa na uzuiaji wa Bangala.

Bangala amecheza maeneo mawili tofauti ya uwanja kwa ubora mkubwa sana. Mechi nyingi amecheza kama kiungo mzuiaji na baadhi ya siku alicheza beki wa katikati. Katika maeneo yote Bangala amecheza katika ubora ule ule.

Bangala ameipa Yanga utulivu mkubwa sana eneo la kiungo akiwa sambamba na kina Khalid Aucho. Ameifanya pia Yanga kuwa imara eneo la ulinzi. Uwepo wake umewaongezea ujasiri wachezaji wengi wa Yanga.

Jaribu kufikiria hii nadharia! Mtoe Mayele safu ya ushambuliaji kisha mtoe Bangala eneo la kiungo au ulinzi wa Yanga, unafikiri Yanga itateseka zaidi ikimkosa nani? Yanga itateseka bila Mayele lakini si kama ambavyo itateseka bila Bangala. Kwa sababu hiyo nafikiri mchezaji bora wa msimu anastahili kuwa Bangala.


Mwisho kabisa niwapongeze TFF kwa kuandaa tuzo mapema tu msimu ulipotamatika. Wachezaji wapate tuzo zao wakiwa bado na kumbukumbu ya msimu husika.

Tuzo zitolewe kabla wachezaji hawajaweka malengo ya msimu mpya pia wapate nafasi ya kuzishukuru timu walizopo ikitokea wanahama.

Kule England hizi sherehe hufanyika wiki mbili kabla ya msimu kutamatika. Lakini baada ya pongezi, vipo baadhi ya vitu vya kuendelea kuboresha.

Kwa mfano, hakuna sababu ya kuficha bao bora la msimu, tangaza mabao yanayowania tuzo hiyo kama inavyokuwa kwa mchezaji bora.

Hakuna pia shida ya kutangaza tuzo za heshima kabla ya siku ya tukio.

-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad