Majibu ya Vipimo vya Ukimwi Yalivyovunja Uchumba..

Nafasi za Ajira Zilizotangazwa Leo Bonyeza Hapa
Majibu ya Vipimo vya Ukimwi Yalivyovunja Uchumba..


Mahakama Kuu, imeyatupa madai ya kulipwa fidia ya zaidi ya Sh550 milioni yaliyofunguliwa na Richard Wamboga, akidai maabara ya kimataifa ya Lancet jijini Dar es Salaam ilimpa majibu kuwa ana Ukimwi wakati alikuwa hana maambukizi.


Katika kesi ya madai namba 124 ya 2022, Wamboga alikuwa anadai kuwa vipimo hivyo ambavyo alipima yeye pamoja na mchumba wake Mei 12, 2021, ilikuwa ni maandalizi ya kufunga pingu za maisha Januari 2022, lakini majibu hayo yalimkimbiza mchumba wake.


Hivyo kupitia kwa wakili Ngusa Erasto, mdai huyo ambaye ni mfanyakazi wa benki ya Azania, akafungua madai dhidi ya maabara hiyo ya Lancet iliyopo katika nchi 14 za Afrika ikiwamo Tanzania, akidai fidia hiyo akiituhumu kwa uzembe na kukosa weledi.


New Content Item (1)


Maabara ya kimataifa ya Lancet ipo katika vituo 170 katika nchi za Botswana,Eswatini, Ethiopia, Gabon, Ghana, Ivory Coast, Kenya, Mozambique, Nigeria, Rwanda, Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe na Tanzania ipo katika majiji na miji mbalimbali.


Katika majibu yao, mdaiwa wa kwanza ambaye ni maabara ya Lancet na mjibu maombi wa pili ambaye ni mkurugenzi mwendeshaji wa maabara hiyo wakitetewa na wakili Prisca Nchimbi, walikanusha madai hayo na kueleza kuwa tuhuma hizo zilitengenezwa.


Hukumu ya Jaji ilivyokuwa


Hata hivyo, katika hukumu aliyoitoa Mei 5, mwaka huu, Jaji Stephen Magoiga wa Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam alisema kesi hiyo haikuthibitishwa katika viwango vinavyokubalika katika kesi za madai hivyo ameitupa na mdai atalipa gharama za kesi.


Jaji Magoiga alisema kwa macho ya kisheria na kwa kuzingatia ushahidi wa pande zote mbili, mdai katika shauri hilo hajaweza kuwasilisha ushahidi kuthibitisha kuwa utaratibu wa vipimo na ushughulikiaji wa majibu hakufuatwa kisawasawa na wadaiwa.


Katika kufikia hitimisho hilo, Jaji alitoa sababu tano, moja ni kuwa mdai alikuwa ni mteja aliyeenda hapo bila rufaa na kwamba licha ya kuonyesha majibu katika taasisi nyingine kuonyesha hakuwa na ukimwi, hakueleza ni namna gani wadaiwa walikuwa wazembe.


Sababu ya pili ni kuwa mdai alikuwa akichanganya ushauri nasaha kabla ya kufanyiwa vipimo na taratibu za kisayansi zinazotumika kabla ya upimaji sampuli kwa ajili ya virusi vya Ukimwi kuanzia kifaa kimoja hadi mwisho majibu ya kimaabara yanapotolewa.


“Uzembe na kukosa weledi kungeweza kujitokeza tu kama majibu yangetokana na kuchanganywa kwa sampuli au kupimwa na mtu ambaye sio mtaalamu,”amesema Jaji katika hukumu yake hiyo ambayo gazeti hili lina nakala yake.


Jaji akaongeza kusema suala la ushauri nasaha ni kitu kingine ambacho kinapaswa kushughulikiwa tofauti na taratibu za upimaji sampuli za Ukimwi na kwamba ushauri hufanywa na daktari, mwanasaikolojia lakini vipimo hufanywa na mtaalamu.


Katika sababu ya nne, Jaji amesema mdai alishindwa kuelezea katika ushahidi wake ni utaratibu upi wa upimaji na ushughulikiaji wa sampuli ambao haukufuatwa na mdaiwa lakini hata shahidi wake alishindwa kueleza nini ambacho hakikwenda vizuri.


Sababu ya tano kwa mujibu wa Jaji ni kuwa mdai aliieleza mahakama kuwa siku hiyo hiyo baada ya majibu alilalamika na vipimo vikarudiwa lakini hapakuwepo majibu ya upimaji huo wa pili yaliyotolewa kortini na kufanya hadithi nzima kuwa ya shaka.


Ukiacha sababu hizo, Jaji amesema muda wote mdai alikuwa akimtaja mchumba wake lakini hata huyo mchumba wake huyo hakuwahi kuitwa mahakamani kutoa ushahidi ili kuunga mkono hadithi ya mdai na hakukuwa na maelezo ya kwanini hakuitwa.


“Mdai alitoa madai ya jumla tu kuwa amepata hasara kwa sababu huyo mchumba anayeitwa Eveline walikuwa tayari wameanzisha mradi lakini hakueleza ni mradi hadi na una uhusiano gani na shauri lililopo mahakamani,”alieleza Jaji Magoiga.


Jaji amesema kama mdai alikuwa na tatizo na majibu hayo ya Ukimwi, angeweza kulalamika kwa menejimenti siku ile ile amepokea majibu au siku inayofuata lakini alichokifanya kinaacha maswali mengi kwani aliamua kwenda kupima sehemu nyingine.


Madai ya majibu yalivyokuwa


Katika madai yake, mdai Richard Wamboga aliiomba mahakama iwaamuru wadaiwa wamlipe fidia ya Sh250,000,000 kwa kile alichodai ni uzembe na kukosa weledi na Sh300 milioni kama fidia ya jumla, wameombe radhi na walipe gharama za kesi hiyo.


Msingi wa madai yake ni kwamba Januari 1,2022 alikuwa afunge ndoa na mchumba wake aliyemtaja kwa jina la Eveline na kama moja ya maandalizi ya ndoa hiyo, Mei 12,2021 waliamua kwenda kwenye maabara ya Lancet jijini Dar es Salaam kupima Ukimwi.


Baada ya kulipia gharama iliyotakiwa na kuchukuliwa sampuli, waliamua kufuatilia majibu siku inayofuata ambapo mfanyakazi wa mapokezi aliwapa majibu kwenye bahasha mbili tofauti na ilionyesha mdai pekee ndio ana maambukizi ya ukimwi.


Kutokana na mshtuko alioupata, aliamua kurudia kipimo hicho na majibu yalikuwa ni sawa na ya awali ndipo akaamua kupima upya kwenye taasisi nyingine ikiwamo hospitali ya IST Masaki, Regency, Sali International na Muhimbili na kukutwa hana Ukimwi.


Baada ya kupata majibu hayo, Juni 20, 2021 alirudi tena maabara ya Lancet na kufanya tena vipimo kwa kutumia jina tofauti na majibu yalionyesha hana Ukimwi na kwamba hiyo inathibitisha wadaiwa walifanya uzembe na hawakuzingatia weledi katika kazi yao.


Alieleza kuwa makosa hayo ya majibu yalisababisha ampoteze mchumba wake kwani uhusiano ulivunjika na mipango ya harusi ilikufa, alipata msongo wa mawazo na kupoteza matumaini ya kuishi na makosa hayo yalimshushia hadhi na heshima.


Walichojibu Lancet


Shahidi pekee wa upande wa wadai, Alista Osiro ambaye ni mtaalamu wa teknolojia ya utabibu kutoka Lancet ambaye alielezea kwa kirefu namna wanavyompokea mhitaji, kuchukua sampuli na kuzichambua kabla ya kuzipeleka maabara kwa upimaji.


Baada ya majibu kupatikana kutoka maabara, majibu hayo huhakikiwa na mtaalamu aliyebobea na baadaye mteja hupewa majibu yake kama ni yeye mwenyewe alihitaji kupima na kwamba majibu hayo huwekwa kwenye bahasha ambayo hufungwa.


Aliieleza mahakama kuwa kutokana na mazingira hayo, jukumu la kutafsiri majibu sio wajibu wao kwani jukumu lao ni kupima tu na kukabidhi kwa aliyehitaji huduma hiyo kama ambavyo Wamboga alivyohitaji kupima Ukimwi.


Osiro amesema madai ya Wamboga hayana msingi kwani walitimiza wajibu wao kwa weledi na kwa uangalifu mkubwa na kwamba wanalo daraja la kwanza la utoaji wa huduma za maabara kitaifa na kimataifa na madai ya uzembe hayana msingi.


Ameongeza katika miaka yake 12 aliyofanya kazi na maabara ya Lancet, hajawahi kukutana na tukio kama la Wamboga na kusisitiza mdai alipaswa kupeleka madai yake kutoka kwa wafanyakazi wa chini hadi menejimenti na wao hawana malalamiko.


Kuhusiana na suala lililo mbele ya mahakama, Osiro amesema walilifahamu jambo hilo baada ya kupokea barua ya madai (demand note) na wala hakuwa anajua nani alimhudumia mdai siku hiyo wala hafahamu ni nani alikuja kupokea majibu.


Akidodoswa na wakili wa mdai, shahidi huyo amekiri kuwa hana ushahidi kuwa jambo hilo ni la kutengenezwa na alipoonyeshwa nyaraka yenye majibu hayo alikiri pia kuwa yanaonyesha kweli ana maambukizi (positive) na majibu ni ya Richard Wamboga.

_________

LOVE STORY YA UTANIKUMBUKA NEYLA Ipo tayari ni maandishi na Sauti !, Kuisoma yote Bonyeza HAPA Lipia tsh 1000 Tu mtandao wowote,au Tembelea www.makapedia.com

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad