11/13/2018

Rais Magufuli Ahudhuria Misa Ya Kushukuru Rais Mstaafu Benjamini Mkapa Kutimiza Miaka 80

Rais Magufuli Ahudhuria Misa Ya Kushukuru Rais Mstaafu Benjamini Mkapa Kutimiza Miaka 80
Rais John Magufuli amempongeza Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa kwa mchango mkubwa alioutoa wakati wa uongozi wake na kueleza Watanzania wataendelea kumkumbuka.

Rais Magufuli ametoa pongezi hizo jana Jumatatu Novemba 12, 2018 wakati wa  misa takatifu ya shukrani ya uhai kwa Mkapa ambaye ametimiza miaka 80 tangu kuzaliwa iliyofanyika katika Parokia ya Bikira Maria Imakulata, Upanga Jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Rais Magufuli alisema wakati akiwa madarakani Mkapa alifanya mambo mengi na muhimu kwa Taifa na amebainisha Watanzania wataendelea kumkumbuka kwa kazi nzuri aliyoifanya.

“Rais mstaafu Mkapa wakati wa uongozi wako ulifanya kazi kubwa na kwa miaka ambayo nilifanya kazi na wewe baada ya kuniteua kuwa naibu waziri na baadaye waziri nilijifunza kuwa wewe ni mcha Mungu, mwadilifu, mnyenyekevu kwa Mungu na mchapakazi.”

“Leo unapotimiza miaka 80 nakushukuru na kukupongeza sana, nakuombea mwenyezi Mungu aendelee kukupa afya njema wewe na familia yako na sisi viongozi tuliopo sasa tutaendelea kuyaenzi mazuri yote uliyoyafanya” alisema Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Mkapa alimpongeza Rais Magufuli kwa uongozi wake kwa kuwa Tanzania imeendelea kuwa na sifa nzuri ya amani na umoja na kwamba hata akiwa nje ya nchi anapoulizwa siri ya Tanzania kuwa na marais wastaafu watatu ambao wanaishi vizuri nchini mwao, huwajibu siri kubwa ni uwepo wa amani, umoja na mshikamano.

Pia amemshukuru Rais  Magufuli kwa kumtakia heri, amewashukuru maaskofu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mwandamizi Jude Thadaeus Ruwai’chi na Askofu Msaidizi Eusebius Nzigirwa walioongoza misa hiyo pamoja na viongozi wengine na waumini wenzake.

Misa hiyo imehudhuriwa pia na mke wa Rais Magufuli, Mama Janeth Magufuli na mke wa rais mstaafu wa Mkapa, Mama Anna Mkapa.
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:
Loading...

0 [disqus]:

Post a Comment

Loading...

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL BLOG | Powered by Blogger