Wema Sepetu Jela Inamuita


Wema KWA mara nyingine, jela au Segerea inamuita Malkia wa Bongo Movies, Wema Isaac Sepetu, Risasi Jumamosi limedokezwa. Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya kisheria, Wema anaweza kukabiliwa na kesi ya matumizi ya lugha chafu (matusi) kwa mmoja wa wafuasi wake kwenye ukurasa wake wa Instagram, anayetumia jina la Binti Iddy.

Kabla ya kuangalia vipengele vya kisheria, ilikuwa hivi; katikati ya wiki hii, Wema aliposti picha yake mpya kwenye ukurasa wake wa Instagram, wenye wafuasi zaidi ya milioni 7.6, akitangaza ujio mpya wa kipindi chake cha Cook With Wema, kinachoruka kupitia chaneli yake ya Wema Sepetu kwenye Mtandao wa YouTube.


Watu mbalimbali waliweka maoni yao wakimpongeza, huku wengine wakimkosoa mwonekano wake kwamba umepoteza nuru, kutokana na kukondeana, ambapo shabiki wake huyo alimuandikia; “Lisura limekuwa bayaaa…” Kwa upande wake, Wema alimjibu; “Kama….(tusi kubwa) wako baby wangu…”

Majibu hayo ya Wema, ndiyo yameelezwa kwamba, yanaweza kumuweka matatani, kwani adhabu yake ni pamoja na kwenda jela kati ya miezi sita hadi miaka mitano, au faini ya kati ya shilingi elfu hamsini hadi shilingi laki tatu, au vyote viwili; kifungo na faini.

Kwa mujibu wa mwanasheria maarufu jijini Dar, aliyezungumza na mwandishi wetu, Peter Mwanakatwe, kutoa lugha ya matusi hadharani, ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria za nchi.

Anasema kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, kuna aina tatu za makosa yanayohusu utoaji wa matusi;

 
“Katika kifungu cha 89 cha sheria hiyo, inatamkwa kwamba, mtu yeyote anayetumia lugha ya kudhalilisha, aidha kwa kutamka au kwa ishara dhidi ya mtu yeyote katika hali ambayo inaweza kusababisha uvunjifu wa amani, mtu huyo atakuwa ametenda kosa la jinai na atakapotiwa hatiani, atatumikia adhabu ya kifungo cha miezi sita jela.“Pia katika kifungu cha 135 cha sheria hiyo, inatamkwa kwamba, mtu yeyote atakayemdhalilisha mtu yeyote kwa kumbughudhi, aidha kwa kutumia maneno, sauti, ishara au kitu kitakachoashiria matusi, na endapo atapatikana na hatia kwa kosa hilo, atapewa adhabu ya kifungo cha muda wa miaka mitano au kulipa faini ya kiasi kisichozidi shilingi laki tatu au adhabu zote mbili kwa pamoja.“Halafu pia, kwenye kifungu cha 138 D inatamkwa kwamba, ni kosa la jinai kwa mtu yeyote kufanya udhalilishaji wa kijinsia kwa mtu mwingine.Mtu yeyote mwenye dhamira ya kutenda uovu, endapo atamshambulia mtu yeyote, aidha kwa maneno au vitendo kwa nia ya kumuudhi au kumdhalilisha kijinsia, mtu huyo atakuwa ametenda kosa na endapo atatiwa hatiani, atapewa adhabu ya kifungo cha miaka mitano au kulipa faini ya shilingi laki mbili au kupewa adhabu zote mbili.“Lakini pamoja na adhabu hizo, mahakama inaweza kumuamuru mshitakiwa aliyetiwa hatiani, kumlipa fidia mlalamikaji.“Tunafahamu makosa yote yanayohusu matusi au udhalilishaji, huweza kutendwa na mtu yeyote bila kujali jinsia yake au umri.“Kwa hiyo, pamoja na makosa yanayohusu lugha ya matusi kuwemo katika sheria za nchi na adhabu zilizopo, bado sheria haiwezi kufanya kazi bila mtu aliyetendewa kosa au makosa ya aina hiyo, kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola vyenye mamlaka ya kushughulikia makosa hayo, hivyo ni jukumu la huyo aliyetukanwa na Wema (Binti Iddy) kwenda kwenye vyombo vya dola kutoa taarifa.“Endapo atafanya hivyo, ndipo Wema anaweza kuingia matatani,” alifafanua mwanasheria huyo. Mwaka 2018, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar, ilimhukumu Wema kwenda jela mwaka mmoja baada ya kupatikana na hatia katika kesi yake ya kukutwa na kutumia dawa za kulevya aina ya bangi, ambapo alilipa faini ya shilingi milioni mbili za Kitanzania na kuachiwa huru. That Gal ya Rosa Ree Yawa Gumzo Itazame Hapa chini:

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO

Post a comment

0 Comments