10/01/2020

Mshukiwa Mauaji ya Kimbari Kushtakiwa Tanzania



MAHAKAMA ya rufaa nchini Ufaransa imekubali kumpeleka mshukiwa wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, Felicein Kabuga, kushtakiwa nchini Tanzania.

Kabuga alikamatwa nyumbani kwake nje ya mji wa Paris baada ya miaka 26 kama mtoro.

Takriban watu 800,000 waliuawa nchini Rwanda katika mauaji ya kimbari ya 1994 ambapo Kabuga anadaiwa kuyapatia makundi ya wapiganaji fedha alipokuwa mwenyekiti wa kitaifa wa hazina ya ulinzi ya kitaifa.

Hata hivyo, amekana madai yote hayo wakati wa kusikilizwa kwa kesi yake mwezi Mei mwaka huu ambapo alielezea madai hayo kama ya uwongo.

Kwa nini anashtakiwa?

Kabuga anashtakiwa kwa kufadhili mauaji ya kimbari nchini Rwanda. Anadaiwa kuwasaidia wapiganaji wa kabila la Wahutu ambao waliwaua takriban raia wa Kitutsi 800,000 pamoja na Wahutu walio na msimamo wa kati 1994.

Alianzisha kituo cha habari cha redio Télévision Libre des Mille Collines (RTLM), ambacho kilidaiwa kutoa wito kwa watu kuwaua watu wa kabila la Watutsi.

Mwaka 1997 alishtakiwa kwa mashtaka saba ikiwemo mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu na jopo la kimataifa lililokuwa likichunguza mauaji hayo.

Alikwepa vipi mtego wa polisi?


Maafisa wa polisi wanasema kwamba Kabuga alitumia majina 28 tofauti kujificha. Akiwa mtoro, alidaiwa kuishi katika mataifa mbalimbali Afrika mashariki ikiwemo Kenya, ambapo yeye na familia yake walikua na biashara. Mwendesha mashtaka wa Ufaransa alisema kwamba amekuwa akiishi kupitia utambulisho bandia.

Mahakama Arusha ni ipi?

Miezi kadhaa baada ya mauaji hayo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilianzisha mahakama ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda mjini Arusha, kaskazini mwa Tanzania. Lengo lake ilikuwa kuwashtaki viongozi wa mauaji hayo na zaidi ya watu 60 walihukumiwa.

Mahakama hiyo ilifungwa rasmi mwaka 2015 na baadaye utaratibu wa Mahakama za Kimataifa za Jinai MICT ulichukua usimamizi wake ili kuwasaka washukiwa wa mwisho.

Mahakama hiyo haina maafisa wa polisi wala uwezo wa kukamata, na badala yake imekuwa ikitegemea serikali tofauti kuchukua hatua hizo badala yake.

Filicien Kabuga ni nani?


Ndiye aliyekuwa mtu tajiri zaidi nchini Rwanda kabla ya mauaji ya 1994. Akijipatia utajiri wake kupita biashara ya majani ya chai mwaka 1970 na alifanya biashara katika sekta chungu nzima nyumbani na katika mataifa ya kigeni.

Alikuwa mshirika wa karibu wa chama tawala cha MRND – na alikuwa na uhusiano na rais wa zamani Juvenal Habyarimana ambaye alifariki 1994. Akituhumiwa kwa kuwa mfadhili mkuu wa mauaji hayo na kutumia biashara yake na uwezo wake kupanga na kufadhili mauaji

Mmiliki wa kituo cha redio ya kibinafsi RTLM alishutumiwa kwa kuwachochea watu wa kabila la Wahutu kuwaua Watutsi. Mwaka 2006, jopo la kimataifa la Rwanda lililokuwa likichunguza mauaji hayo lilisema lina ushahidi kwamba bwana Kabuga alizuru nchini Kenya ama hata kuishi nchini humo, ambapo alikuwa akisimamia maslahi yake ya kibishara.

Miaka mitatu baadaye, Stephen Rapp, ambaye alikuwa balozi wa Marekani aliishutumu serikali ya Kenya kwa kukataa kumtoa Kabuga. Kulikuwa na ushahidi kwamba Kabuga alihudhuria hafla zilizoshirikisha watu maarufu, alisema madai ambayo Kenya imekana.

Ni wazi kwamba familia ya  Kabuga ilikuwa ikimiliki mali nchini Kenya baada ya mali moja kuzongwa na kesi 2015 wakati mkewe, Josephine Mukazitoni, ambaye alikuwa mmiliki mwenza, alipojaribu kuimiliki.

Matembezi wakati wa amri ya kutotoka nje

Majirani zake wanasema mzee huyo aliishi katika eneo hilo kwa takriban miaka mitatu hadi minne. Olivier Olsen, kiongozi wa muungano wa wamiliki wa nyumba katika mtaa huo aliokuwa akiishi, aliambia AFP kwamba Kabuga alikuwa msiri mkubwa na mtu aliyetoa matamshi kwa kunong’ona alipokuwa akisalimia.

Kabla ya amri ya kutotoka nje alionekana akifanya matembezi ndani ya mtaa huo, alisema.  Kabuga kwa sasa anazuiliwa katika jela ya La Sante katikati mwa mji mkuu wa Paris, ambapo atasalia hapo hadi atakapohamishwa na kuwa mikononi mwa IRMCT.


Hata hivyo, wakili wa Kabuga amesema kwamba mteja wao angependelea kufunguliwa mashtaka nchini Ufaransa. Manusura wa mauaji hayo ya kimbari wanatumai kwamba kesi hiyo haitachukua muda na kwamba haki itapatikana kwa haraka.


Baada ya kukamatwa kwake Valerie Mukabayire, kiongozi wa wajane nchini Rwanda, aliambia BBC kwamba kila manusura wa mauaji hayo ya 1994 nchini Rwanda anafurahia kukamatwa kwake.


 Kila mtu amekuwa akisubiri habari hizi. Ni kitu kizuri kwamba atakabiliwa na mkono wa sheria,” alisema.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:
Loading...

0 Blogger:

Post a comment

Loading...

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL BLOG | Powered by Blogger