Panya wafukua mbegu zilizopandwa Kibindu
Na Omary Mngindo, Bagamoyo
WAKULIMA katika vijiji vinavyounda Kata ya Kibindu Halmashauri ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wanakabiliwa na changamoto ya panya wanaofukua mbegu zinazopandwa.

Hali hiyo inasababisha usumbufu mkubwa kwa wakulima hao, ambao wanalazimika kurudiarudia kupanda mbegu zaidi ya mara moja au mbili hali inayowaongezea hasara ya kuzinunua kisha kuzipanda tena.

Hayo yamebainishwa na Diwani Mteule wa Kata hiyo Ramadhani Mkufya, akizungumza na Waandishi wa habari Lugoba ambapo alisema hali hiyo imekuwa tatizo kubwa, na kwamba tayari Halmashauri wameshaanza kulifanyiakazi.

"Ujio wa mvua ni faraja kwetu sisi wakulima, lakini kwa mwaka huu wameibuka panya waharibifu ambao wanafukua mbegu za mahindi zinazopandwa, hali hiyo inasababisha usumbufu na hasara kwa wakulima," alisema Mkufya.

Alisema kwamba tayari wameshawasiliana na Wataalamu wanaohusika na kilimo ambao walifika ofisi ya Kata, na kueleza kuwa wanakwenda kulifanyiakazi suala hilo ili wakulima hao waweze kuendelea na shughuli zao za upandaji.

"Niwaombe wakazi wa Kibindu wawe watulivu, suala la uvamizi wa panya tumeshaanza kulifanyiakazi, wahusika walifika ofisi zetu za Kata tukawaelezea changamoto yetu, wameahidi wanakwenda kulifanyiakazi," alisema Mkufya.

Alimalizia kwa kuishukuru ofisi ya Mkurugenzi chini ya Ramadhani Posi kwa namna anavyoitumikia vyema ofisi hiyo, ambapo katika kipindi kifupi tangu aripiti Chalinze kazi kubwa ameshaanza kuifanya, hali inayoleta faraja kwa wana-Chalinze.


HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO

Post a comment

0 Comments