Mondi Atamtoa Harmo Roho …Mashabiki Wafunguka

 


ANAWEWESEKA! Ndivyo mashabiki wa muziki wa Bongo Fleva nchini wanavyomtafsiri msanii wa muziki huo, Rajabu Abdul ‘Harmonize’ ambaye ameendelea kujinasibu kuwa ndiye msanii namba moja nchini.

Tambo hizo za Harmo zimekuja ikiwa ni miezi 15 imetimia tangu alipoondoka kwenye lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), iliyopo chini ya Msanii maarufu nchini, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

Hata hivyo, tangu ajinasue kwenye lebo hiyo na kwenda kuanzisha lebo yake aliyoipatia jina la Konde Gang, Harmonize amedaiwa kuteswa na Mondi kitendo ambacho mashabiki wanasema sasa kitaweza ‘kumtoa roho’.

Harmo ambaye awali alikiri kuwa Mondi ndiye ‘role modal’ wake, aliibuliwa na kukuzwa kimuziki na WCB jambo ambalo mashabiki wa muziki bado wanamtazama Mondi kama baba yake kimuziki….

ATESEKA

Mashabiki wa msanii huyo wamemuelezea Harmo kuwa anateseka katika kuhakikisha anamfikia Mondi kwa kila jambo kitu ambacho kimetafsiriwa kuwa si jambo rahisi kwa msanii huyo kufanya hivyo.

Kauli za mashabiki hao zimekuja baada ya Harmo kurusha video mbili katika mtandao wake wa Instagram zikimuonesha akiwa amembeba mtoto wa kike aliyedai kuwa ni mwanaye kisha kupiga vijembe kuwa yeye ni namba moja.Video hizo zimetafsiriwa na mashabiki kuwa, Harmo anatumia nguvu kubwa kumtengenezea umaarufu mtoto huyo aliyedai ni wa kwake, licha ya kujawa na utata wa kila aina.

“Hawezi kumfikia Tiffah, Harmo anahangaika sana kutafuta kiki. Kiki zitakutoa roho kwa sababu kumfikia Mondi ni ndoto,” aliandika shabiki mmoja katika mtandao huo na kuungwa mkono na wenzie.

Kauli za mashabiki hao zilitokana na maneno ya Harmonize katika video hiyo ambayo ilimuonesha ‘kuzuga’ kumbembeleza mtoto huyo aliyetaka kuangulia kilio wakati amembeba na kusema;“Nani amekuudhi, nani Baba Levo… achana naye, walianza kina Dudubaya wakashindwa, achana naye. You are safe, i love you so much.

Your dad is a number one Tanzania artist right now. You have to be proud, let us go and work hard, lets make music mamaa.”

SAUTI Harmo ameonekana kuendelea kuteswa na Mondi tangu alipotusua na ngoma yake ya ‘Bado’ ambapo ndani yake alimshirikisha Mondi. Ndani ya ngoma hiyo na nyingine zote zilizofuatwa Harmo alilaumiwa na mashabiki kuiga sauti ya Mondi jambo ambalo walidai lingeweza kumwangusha kimuziki.Hata hivyo, Harmo mara kwa mara alikuwa akikanusha madai hayo na kufafanua kuwa anaimba kwa kutumia sauti yake halisi.

MAVAZI NA LIFESTYLE

Wakati akiwa WCB, Harmo alionekana kutembea katika mapito yote ya Mondi, ikiwamo mavazi na hata mtindo wa maisha na mahusiano. Hilo lilidhihirishwa na mahusiano yake na wanawake waliomzidi umri kama Mondi alivyofanya kwa akina Wema Sepetu na Zarinah Hassan ‘Zari the Boss Lady’ ambapo matokeo yake Harmo naye aliangukia katika penzi la Jackline Wolper.

Wakati Mondi akihamishia majeshi kwa vimwana wa nje ya nchi, Harmo naye alizama kwenye penzi la raia wa Italia, Sarah Michelotti ambaye walidaiwa kufunga ndoa kabla ya hivi karibuni kudaiwa kuwa wameachana.

Kutokana na hali hiyo, mashabiki wa muziki huo nchini, wameendelea kusisitiza kuwa msanii huyo, atumie kipaji na uweledi wake bila kulazimisha kushindana na Diamond.“


Sawa ushindani ni jambo zuri, lakini anatakiwa kuangalia na nyakati, huwezi kushindana na Mondi kwa staili ile ya kuposti video na kuwachamba wasanii wenzake,” aliandika mmoja wa wafuasi wake kwenye mtandao huo wa Instagram.

Mwandishi Wetu, Risasi


 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO

Post a comment

0 Comments