Imefichuka: Melinda Gates Alianza Kusaka Talaka Tangu 2019
SIKU chache baada ya wanandoa matajiri zaidi duniani, Bill Gates na mkewe Melinda Gates kutangaza kwenye akaunti zao za mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba penzi lao limefika mwisho, imebainika kwamba kumbe mwanamke huyo, alianza mchakato wa kudai talaka tangu 2019.

 

Gazeti la Daily Mail la nchini Uingereza, limefichua kwamba linao ushahidi wa madai hayo na hatua hiyo ilichukuliwa na Melinda kutokana na ukaribu wenye kutia shaka kati ya mumewe na mfanyabiashara mwingine mkubwa, Jeffrey Epstein ambaye kwa sasa ni marehemu.


Inaelezwa kwamba Melinda aliwahi kunukuliwa na Jarida la Wall Street Journal mwaka 2019 akieleza kwamba ndoa yao ilikuwa ikielekea kuvunjika na tangu kipindi hicho, amekuwa akishirikiana na wanasheria wake wakiongozwa na Robert Stephan Cohen kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa katika mchakato wa kupeana talaka.

 

Epstein, alifariki mwaka huohuo, 2019 kwa kujinyonga akiwa gerezani ambapo alikuwa akikabiliwa na mashtaka ya kumdhalilisha binti mdogo kingono pamoja na mashtaka mengine ya unyanyasaji wa kingono ambapo inaelezwa kwamba kabla ya kifo chake, alisafiri na Bill Gates kwa kutumia ndege binafsi kwenda katika Fukwe za Palm Beach, Florida, jambo ambalo mwanamke huyo hakulifurahia.

 

Ukaribu wa Bill Gates na Epstein ulianza mwaka 2013 na inaelezwa kuwa mkewe hakuwa akifurahia ukaribu wao na alishamuonya mumewe mara kadhaa, hasa ikizingatiwa kwamba Epstein amewahi kutumikia kifungo gerezani kwa makosa ya udhalilishaji wa watoto kingono.

 


HABARI HIZI ZINAPATIKANA  KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO BURE