.

5/25/2021

Kigogo mpya Bawacha afichua siri tatu kina Mdee kuapishwa 
Mwanza. Kwa wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa nchini, Chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema), chini ya uongozi wa Freeman Mbowe ni kati ya vyama vya siasa vyenye uzoefu wa kukabiliana na kuvuka salama misukosuko mbalimbali ya kisiasa tangu mfumo wa vyama vingi uliporejea mwaka 1992.

Miongoni mwa misukosuko hiyo ni pamoja ajali iliyosababisha kifo cha aliyekuwa makamu mwenyekiti, Chacha Wangwe, kuvuliwa uanachama kwa aliyekuwa naibu katibu mkuu (Bara), Zitto Kabwe na kukimbiwa kwa makada na viongozi wenye ushawishi akiwemo aliyekuwa Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa, wabunge na wajumbe kadhaa wa kamati kuu waliohamia CCM.

Tangu Novemba 24, mwaka jana Chadema inapita kwenye mtanziko mwingine wa waliokuwa viongozi na wanachama wake 19 kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu katika Bunge la 12 kinyume na msimamo wa chama hicho.

Tukio hilo lilikuwa la kushtukiza na wabunge hao kuapishwa nje ya ukumbi wa Bunge, tena wakati ambapo hakuna mkutano wa Bunge unaoendelea, jambo lililotetewa na spika Job ndugai kuwa limefanya kikanuni baada ya kanuni kufanyiwa marekebisho.


 
Walioapishwa katika mazingira hayo na baadaye kuvuliwa uanachama wa Chadema tangu Novemba 27, mwaka jana ni Halima Mdee, Grace Tendega, Esther Matiko, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Jesca Kishoa, Nagenjwa kaboyoka, Anatropia Theonest, Salome Makamba, Conchesta Rwamlaza.

Wengine ni Agnesta Lambart, Nusrati Hanje, Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala na Stella Fiao.

Japo wameendelea kuwa bungeni baada ya Spika Ndugai kukataa kutambua barua ya inayomtaarifu uamuzi wa wabunge hao kuvuliwa uanachama kwamba ilikosa viambatanisho muhimu, Chadema imeendelea kutekeleza michakato kadhaa ya kuwaondoa kwenye mfumo wa uongozi ikiwemo nafasi zao ndani ya Bawacha na Bavicha kuzibwa.


Miongoni mwa walioziba nafasi hizo ni Catherine Ruge, katibu mkuu mpya wa Bawacha akijaza nafasi iliyoachwa wazi na Grace Tendega, ambaye amezungumza na Mwananchi na kufichua mambo matatu anayoamini yaliwasukuma Mdee na wenzake kufikia uamuzi huo aliosema ni usaliti kwa chama, dhamira na malengo yao waliyoyapigania kwa kipindi kirefu.

 Kukata tamaa

“Licha ya kupitia katika mchakato mgumu uliojaa hila na ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu, matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 yaliwakatisha tamaa viongozi, wanachama, wafuasi na wapenzi wa vyama vya upinzani pamoja na wapenda mageuzi wote.

“Ilihitajika ustahimilivu na dhamira ya dhati kukubaliana na kilichotokea na kuendelea kupigania imani yetu,” alisema Ruge.

Katibu mkuu huyo aliyekuwa mbunge wa viti maalumu katika Bunge la 11 kabla ya kugombea ubunge jimbo la Serengeti mwaka 2020, alisema miongoni mwa walioapishwa bila ridhaa ya chama ni wabunge wa majimbo na viti maalumu waliowekeza karibia fedha zote za kiinua mgongo kwenye kampeni za uchaguzi wakiwa na uhakika wa kushinda lakini matokeo yakawa kinyume cha matarajio yao.


 
“Walijikuta wakiwa desperate (wamekata tamaa) wakifikiria mamilioni ya fedha waliyopoteza kwenye mchakato wa uchaguzi ndani na nje ya chama. Katika kundi hilo wapo viongozi waliojijengea heshima ndani na nje ya chama kwa uwezo wao. Lakini walishindwa kuhimili desperation na kunasa kwenyemtego wa kuapishwa bila ridhaa ya chama,” alisema Ruge.

Huku akiweka wazi kuwa yeye binafsi alitumia zaidi ya Sh150 milioni katika mchakato wa kampeni huku akiwataja baadhi ya waliokuwa wabunge waliotumia zaidi ya Sh200 milioni za kiinua mgongo chao cha ubunge kwenye kampeni, Ruge alisema hata hivyo hakuna gharama wala kiwango cha fedha kinacholingana na imani wanayopigania wapenda demokrasia nchini.

 “Ni bahati mbaya sana kwamba wenzetu wamekubali kuisaliti cause (nia) tuliyopigania kwa miaka yote. Wamekisaliti chama na wamesaliti pia nafsi zao wenyewe. Hii ndiyo tofauti na ugomvi wangu mimi na wao,” alisema.

Hofu ya kukosa

“Tangazo la NEC (Tume yaTaifa ya Uchaguzi) kuwa Chadema ina nafasi 19 za wabunge wa viti maalumu liliibua hofu ya namna gani nafasi hizo zitagawanywa kukidhi uwiano kimikoa, uwakilishi wa makundi ya kitaaluma, uzoefu kiungozi na uwezo binafsi wa kujenga na kutetea hoja,” alisema Ruge, ambaye kitaaluma ni mhasibu.


Bila kutaja vigezo vilivyowekwa na Chadema, Ruge alisema hofu ya kutoamini kupata nafasi na hulka ya kuweka mbele masilahi binafsi kuliko taasisi ni sababu nyingine iliyowasukuma baadhi ya waliokuwa wana Chadema kukubali kuapishwa bila ridhaa ya chama.

Kutojiandaa nje ya ubunge

Kwa mujibu wa Ruge “kuna ugonjwa wa hofu ya maisha nje ya ubunge inayowatesa wabunge wengi, hasa wale ambao hawajawekeza kwenye miradi inayoweza kuwaingizia kipato nje ya ubunge.

“Walioko kwenye kundi hili wako tayari kufanya lolote litakalowapa fursa ya ubunge;

hata kwa kuisaliti imani na nafsi zao wenyewe,” alisema Ruge huku akisisitiza kwamba anawaheshimu waliokuwa wabunge na viongozi wenzake kwa mchango wao wa ujenzi wa chama.

Mikakati ya Bawacha

Pamoja na sababu hiyo, Ruge anasema “tukio la wabunge 19 liliiumiza chama na zaidi Bawacha iliyobakiwa na viongozi wawili pekee baada ya wenzetu sita kusaliti chama.’ Kutokana na hilo, anasema viongozi wapya wana wajibu wa kuijenga upya bawacha kuanzia ngazi ya msingi hadi Taifa.


 
Ruge ambaye kabla ya kukabidhiwa nafasi hiyo alikuwa mweka hazina baraza, anasema “pamoja na ujenzi wa Baraza, Bawacha pia tunalo jukumu kubwa la kuihami Katiba ya nchi kwa kuwashinikiza viongozi walioapa kuilinda kutii viapo vyao; tumeanza na Spika Job Ndugai na uongozi wa NEC kuhusu wabunge 19 walioko bungeni bila kuwa wanachama wa chama chochote cha siasa,” alisema Ruge.

Alitaja kipaumbele kingine cha Bawacha kwa mujibu wa maazimio ya kikoa cha kamati tendaji kilichoketi jijini Mwanza, ni kudai Tume Huru ya Uchaguzi kwa sababu uongozi wa Taifa unapatikana kupitia chaguzi za kisiasa zinazosimamiwa na NEC.

“Kwetu Bawacha tume huru ya uchaguzi ni kipaumbele kuliko hata Katiba mpya; unaweza kuwa nayo lakini usipokuwa na tume huru ni sawa na bure kwa sababu tutaendelea kupata viongozi wanaojiweka au kuwekwa madarakani kinyume cha ridhaa ya wapigakura,” alisema.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:

0 Blogger:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger