.

6/07/2021

Waziri Gwajima ateua watu 10 kuunda kamati ya mpito, Aipa siku 30
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameunda Kamati ya mpito ya Watu 10 wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) na kuipa siku 30 kuhakikisha wanasimamia uchaguzi wa viongozi na wajumbe Baraza la Taifa la Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali(NaCoNGO) kwa mujibu wa kanuni zilizopo.

Hayo ameyasema leo Juni 7,2021 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari  Dkt. Gwajima amesema kuwa kwa mujibu wa Sheria, Viongozi waliopo madarakani katika Baraza hilo muda wao ulikwisha tangu mwaka 2019.

Dkt. Gwajima ameongeza kuwa Baraza hilo limeshindwa kufanya uchaguzi kwa kipindi chote pamoja na kuelekezwa na Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kufanya hivyo kwa muda mrefu.

“Nimeelezwa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali iliwapa Baraza la Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali muda mwingi na nyongeza pia ili kufanya uchaguzi lakini bado hawakutekeleza maagizo hayo” amesisitiza Dkt.Gwajima

Aidha  amefafanua kuwa kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha 38 (1) na (2) cha Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 24 ya mwaka 2002, kuhusu usimamizi wa Sheria hii na utekelezwaji wa kanuni zake, ikiwemo Kanuni za Uchaguzi wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali za mwaka 2016, ameagiza uchaguzi huo ufanyike haraka ili kuwezesha vyombo vya usimamizi wa Mashirika hayo kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria.

“Kwa mamlaka niliyopewa kuhusu usimamizi wa Sheria hii ya utekelezwaji wa Kanuni zake, ikiwemo Kanuni za Uchaguzi wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali naunda Kamati ya mpito ili kuhakikisha Uchaguzi unafanyika haraka kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi zilizopo.” amesema Dkt. Gwajima.

Ameitaka Kamati hiyo kuhakikisha uchaguzi unafanyika haraka iwezekanavyo ili kuwezesha vyombo vya usimamizi wa Mashirika hayo kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria.

Hata hivyo amesema  kuwa Wizara haitavumilia tena watendaji na washirika ambao wanatekeleza wajibu wao kwa kasi isiyoridhisha kwani wanaathiri utekelezaji wa majukumu ya Serikali.

Kamati hiyo ya watu 10 ni inaundwa na Flaviana Charles Mwenyekiti wa Shirika Mtandao la Coalition for Women Human Rights Defenders in Tanzania (CWHRDsTZ).

Francis Kiwanga – Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Foundation for Civil Society (FCS).

Dkt. Tulli Tuhuma – Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la JSI Research and Training Institute (JSI) na

Edward Porokwa – Mratibu wa Shirika Mtandao la Pastoralist Indigineous Non-Governmental Organizations Forum (PINGOs Forum).

Wengine ni Tike Mwambipile – Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Tanzania Women Lawyers Association (TAWLA).

Yassin Ally – Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kivulini Womens Rights Organization (KIVULINI).

Anna Kulaya – Mratibu wa Kitafa wa Shirika la Women in Law and Development Africa (WiLDAF).

Audax Rukonge – Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Agicultural Non State Actors Forum (ANSAF).

Gunendu Roy – Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Kimataifa la BRAC Maendeleo Tanzania (BRAC).

Dkt. Astronaut Bagile – Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Women in Social Enterpreneurship (WISE).


HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:

0 Blogger:

Post a Comment

New Video - Wana Wanywe Pombe

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger