.

9/09/2021

Aliyemrithi Maalim Seif atoa msimamo wa ACT na katiba
 
KIFO cha Maalim Seif Shariff Hamad, kimemuibua Dorothy Semu, ambaye amechukua nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT- Wazalendo, iliyokuwa ikishikiliwa na mkongwe huyo wa siasa za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Dorothy Semu (kushoto ) katika harakati za kumnadi mgombea wa ACT- Wazalendo wakati wa kampeni za kisiasa, kisiwani Pemba. PICHA: MTANDAO
Katika mazungmzo yake na gazeti hili, jijini Dar es Saalam hivi karibuni, pamoja na kushika nafasi hiyo anatamka “pengo la kiongozi huyo halizibika ndani ya chama.”

Anamtaja Maalim Seif Shariff Hamad, alikuwa mfano mzuri katika kukuza na kulea viongozi wengine na kuwafanya wawe na msimamo usioyumba, kama kilivyoonyesha kwenye tozo za miamala ya simu na katiba mpya. Fuatilia mazungumzo ya ana kwa ana:    

SWALI: Kwa wasiomfahamu Dorothy ni nani na historia yako ni ipi katika siasa?

JIBU: Mimi ni mama wa watoto watatu nimezaliwa Kilimanjaro. Kitaaluma ni mtaalamu wa Jiografia na nimelelewa na wazazi waliokuwa watumishi wa serikali.


 
Mimi ni Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Bara na nakaimu cheo cha Mwenyekiti Taifa, baada ya Maalim Seif, kufariki.

SWALI: Unajigawaje kutekeleza majukumu ya kichama na ya mama wa familia?

JIBU: Siasa ni tasnia ambayo inahitaji sana muda wako na ni maisha ya kila siku na inatuathiri katika kila nyanja.


Kwa hiyo, siasa zikiwa nzuri na maisha yetu yatakuwa bora. Kama mama, ninasema siasa inahitaji muda wako, inahitaji pia akili kwa kuwa mwanamke pamoja na kuwa hivyo, unatakiwa uwe kiunganishi na mratibu wa mambo mengi.

Ninachoweza kusema huwa sijitahidi kuwa 'super woman', yaani kuwa ninapika mwenyewe, ninafua mwenyewe, lakini ninajitahidi kuwa mratibu mzuri wa yale mambo yote ninayotakiwa kuyafanya.

Ninatakiwa kuwa mama, hivyo ninafanya kazi yangu ya mama nyumbani, lakini pale ambapo ninaona ninahitaji msaada au msaidizi, sijinyimi hiyo nafasi, ninajitahidi kuwa na wasaidizi sahihi mahali sahihi.

Na watu wanaonisaidia kazi, sio kwamba nimewaachia majukumu, lakini kuwapo na ule usaidizi ni muhimu, kwa sababu huwezi kubeba kila kitu kwa wakati mmoja, lazima yatakushinda au utaelemewa upande mmoja.


 
Ili uwe mratibu mzuri unahitaji uwe na wasaidizi wazuri, mume wangu ni msaidizi mkubwa kwenye ulezi, kwa hiyo, familia inaenda vizuri.

Ninajitahidi kuwa na watu watakaonisaidia vizuri kwenye siasa kuangalia majukumu yangu ni yapi, kuratibu wale walio chini yangu na kuhakikisha yote yanayotakiwa kufanyika yanafanywa kwa wakati.

Dhana ya kwamba mwanamke unatakiwa uwe 'super woman', ni kweli unakuwa mwanamke wa shoka, lakini lengo sio kubeba kila kitu kwa pamoja kikakulemea. Badala yake ni kuvipangilia na kuratibu, ili vyote vifanyike kwa wakati na ufanikiwe.

Tunawaambia wanawake tuwe wapangiliaji wa mambo, tuyaratibu yaende na wewe majukumu yako muhimu yawe yanakwenda vizuri na tusione ni udhaifu kwa mwanamke kuhitaji wasaidizi. Mwanamke unatakiwa upate wasaidizi bora zaidi, ili kazi zako zifanikiwe zaidi.


SWALI:  Kufariki Maalim Seif kumekiathiri vipi chama?

JIBU: Maalim Seif alikuwa ni gwiji na kungwi wa siasa. Ni mtu ambaye sidhani kama nina maneno ya kumwelezea.

Nilipata nafasi ya kufanya naye kazi kwa miaka hii miwili na katika uwenyekiti wake, alikuwa mfano katika kukuza na kulea viongozi wengine.

Kwa hiyo, kama taasisi tunaweza kusema tumefaidika na uwapo wa Maalim Seif, kwa sababu amezaa watu wengine wengi imara na makini katika ujenzi wa chama chetu.

Tunapungukiwa kumkosa kama sehemu yetu, hekima, busara na ualimu wake, tumepungukiwa sana katika hilo na tunaamini ni pengo, ambalo haliwezi kuzibika.
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:

0 Blogger:

Post a Comment

New Video - Wana Wanywe Pombe

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger