4/21/2022

CAG abaini fedha za mifuko hifadhi ya jamii ziko hatariniMDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amebaini mifuko ya hifadhi ya jamii iko hatarini kupata hasara ya mabilioni ya shilingi kutokana na utekelezaji duni wa miradi yake ya ubia na kampuni mbalimbali.

CAG Charles Kichere.
CAG Charles Kichere anabainisha hayo kwenye ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2020/21 iliyowasilishwa bungeni Jumanne iliyopita, hivyo kuwa wazi kwa umma.

Anasema dosari ya kwanza ameibaini kwenye mradi wa Kiwanda cha Tangawizi cha Mamba Miamba, akifafanua kuwa mwaka 2016, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa LAPF (kwa sasa PSSSF) ulikubaliana na Chama cha Ushirika cha Wazalishaji wa Tangawizi cha Mamba-Miamba kufufua na kukifanya Kiwanda cha Tangawizi cha Mamba-Miamba katika Kijiji cha Mamba Miamba wilayani Same kuwa cha kisasa.

CAG anasema kiwanda hicho kilikuwa kimesimama kutokana na matatizo ya kiteknolojia na kwamba randama ya makubaliano kati ya Chama cha Ushirika cha Wazalishaji wa Tangawizi na LAPF iliyotiwa saini Septemba Mosi, 2020 ilieleza kuwa mfuko utamiliki hisa asilimia 67 na Chama cha Ushirika cha Mamba kitamiliki hisa asilimia 33.

Anasema kuwa hadi kufikia tarehe 30 Juni 2021, mfuko ulikuwa umetumia Sh. bilioni 1.71 kwa ajili ya kufufua kiwanda hicho na shughuli zingine za usimamizi.


 
Hata hivyo, CAG anasema alibaini kuwa hadi Novemba 2021, kiwanda kilikuwa hakijaanza uzalishaji kwa sababu ya kuchelewa kufunga mashine.

"Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma ulieleza kuwa kuchelewa kufungwa kwa mashine za kiwanda hicho kulisababishwa na kuchelewa kusafirisha mashine hizo kutoka kwa mtengenezaji nchini China kutokana kuzuka kwa janga la UVIKO-19 lililosababisha kuwekwa vizuizi vya usafirishaji," anasema.

BIDHAA ZA TIBA

CAG anaitaja dosari ya pili iliyoko kwenye mradi wa Kiwanda cha Bidhaa za Tiba cha Simiyu, akifafanua kuwa tarehe 11 Novemba 2016, Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Benki ya Uwekezaji – Maendeleo (TIB-Development), Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda (TIRDO), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba (TMDA) (zamani Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania-TFDA)walitia saini randama ya makubaliano ya kuanzisha kiwanda cha bidhaa za tiba zinazotokana na malighafi ya pamba katika Kijiji cha Dutwa, Bariadi.


CAG anasema kuwa kwa mujibu wa upembuzi yakinifu uliofanywa na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania, gharama za mradi huo zilikuwa Sh. bilioni 69.21 zitakazogawanywa sawa baina ya wabia."Tarehe 13 Juni 2018, WCF na NHIF walisajili kampuni maalumu ya kuendesha kiwanda hicho.

Ombi la idhini ya uanzishaji wa kiwanda liliwasilishwa kwa Wizara ya Fedha na Mipango tarehe 26 Juni 2019.

"Hata hivyo, nilibaini kuwa hadi Novemba 2021, kiwanda kilikuwa hakijaanza uzalishaji kikisubiri kibali cha Wizara ya Fedha na Mipango. Pia nilibaini kuwa hadi kufikia tarehe 30 Juni 2021, NHIF na WCF walikuwa wametumia kwa usawa Sh. milioni 915 kwa ajili ya kuendeleza kiwanda hicho.

"Gharama hizi zilijumuisha gharama za awali ambazo ni pamoja na gharama za mikutano na gharama za upembuzi yakinifu," CAG Kichere anabainisha katika ripoti yake hiyo.


 
Anasema kuwa dosari nyingine iko kwenye mradi wa Kiwanda cha Chai cha Mponde, akifafanua kuwa mnamo mwezi Januari 2016, serikali ilijimilikisha Kiwanda cha Chai Mponde kutoka cha Wakulima wa Chai Samara (UTEGA) kilichobinafsishwa awali baada ya UTEGA kushindwa kukiendesha kiwanda hicho.

"Kupitia juhudi za Msajili wa Hazina, Septemba 2019, WCF na NHIF waliingia makubaliano ya kufufua Kiwanda cha Chai cha Mponde. Kwa mujibu wa upembuzi yakinifu, mtaji uliohitajika kufufua kiwanda ni Sh. bilioni 4.05 na hisa za kiwanda zingemilikiwa sawa baina ya wabia.

"Katika ukaguzi wangu, nilibaini serikali ilitoa kibali cha uendelezaji wa kiwanda mwezi Machi 2021. Hata hivyo, hadi Novemba 2021 kiwanda kilikuwa hakijaanza uzalishaji kutokana na kusubiri ununuzi wa mashine za kufufua kiwanda na ukarabati wa majengo na mifumo ya maji na umeme. 

"Hadi kufikia tarehe 30 Juni 2021, WCF ilikuwa umetumia Sh. milioni 64 kwa ajili ya gharama za awali za uendelezaji wa kiwanda ambazo ni pamoja na gharama za mikutano na usafiri," anasema.


CAG ana angalizo kwamba kuchelewa kuanza kwa uzalishaji wa viwanda hivyo kunaathiri kufikiwa kwa malengo ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21) uliopangwa kuleta mageuzi ya uchumi kupitia viwanda.

"Ninapendekeza mifuko ikijumuisha PSSSF, WCF, NHIF na NSSF iharakishe kufungwa kwa mashine na kujenga miundombinu husika ili kuanza uzalishaji haraka katika viwanda vilivyoanzishwa au kununuliwa na mifuko hii, na serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango itoe kibali cha kuendeleza Kiwanda cha vifaatiba cha Simiyu," anasema.

USIMAMIZI DUNI 

CAG Kichere analitaja eneo lingine lenye dosari kwa mifuko hiyo kuwa ni usimamizi duni wa kampuni tanzu na kampuni za ubia zinazomilikiwa na mashirika ya umma.

Anasema amebaini ongezeko la mtaji lenye mgogoro katika Kituo cha Uwekezaji cha APC - Bunju, akifafanua kuwa Februari 2, 2015 Mfuko wa Pensheni wa GEPF (kwa sasa PSSSF) uliingia mkataba wa ubia na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) ya kukamilisha na kuendesha kituo hicho.

Anaendelea kubainisha kuwa makubaliano hayo yanaeleza kuwa, asilimia 80 ya faida inayopatikana inapaswa kugawanywa kwa wabia kulingana na umiliki wao na asilimia 20 ya faida iwekwe kama akiba ya kuendesha biashara.


 
"Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Sekta ya Umma ulikuwa umewekeza Sh. bilioni 9.93 ambazo ni asilimia 55.3 ya umiliki wakati NBAA imewekeza Sh. bilioni 8.02 ambayo ni sawa na asilimia 44.7.

"Kituo cha Uwekezaji cha APC kimekuwa kikipata hasara kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo iliyopita (2018/19-2020/21), na kwa mwaka wa fedha 2020/21 kituo kilipata hasara ya Sh. bilioni 2.35 (Sh. bilioni 5.17 mwaka 2019/20).

"Mwenendo huu wa hasara unaleta shaka ya kurejeshwa kwa kiasi kilichowekezwa na wabia. Nilibaini kuwa, NBAA ilikopa Sh. bilioni 15 kutoka (NSSF) ambazo zimedhaminiwa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Uwekezaji cha APC," anasema.

CAG anaendelea kubainisha kuwa kutokana na kituo kushindwa kulipa mkopo, NBAA iliomba mkopo huo kutambulika kama mtaji wa mfuko wa NSSF kwenye kituo hicho.

Hata hivyo, CAG anasema Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Sekta ya Umma ulikataa utaratibu huo kwa madai kuwa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii wa Sekta Binafsi (NSSF) siyo sehemu ya wabia na pia haikuhusika katika kukopa endapo utaratibu huo utakubaliwa basi umiliki wa NBAA upungue kwa kiasi atakachopewa NSSF.

"Ninapendekeza PSSSF na NBAA waharakishe utatuzi wa mgogoro wa nyongeza ya mtaji ili wabia waweze kupata mapato stahiki yanayoendana na uwekezaji walioufanya," CAG anawasilisha hoja yake.

HABARI HIZI ZA UDAKU ZINAPATIKANA KATIKA APP YA UDAKU SPECIAL, IDOWNLOAD>> HAPA BURE 

0 Blogger:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger