4/18/2022

Watumishi Waliotajwa na CAG kukionaWAKUU wa mikoa wameelekezwa kusimamia uchukuaji wa hatua stahiki za kinidhamu kwa watumishi zaidi ya 1,000 waliotajwa kuhusika na kasoro zilizobainishwa kwenye taarifa ya ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kwenye mamlaka za serikali za mitaa.

Agizo hilo lilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Innocent Bashungwa wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi yake kwa mwaka 2022/23.

Alisema Ofisi ya Rais - Tamisemi imeendelea kutoa maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu usimamizi wa fedha kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo inayotolewa mara kwa mara ili kujenga nidhamu ya matumizi ya fedha za umma.

"Lengo ni kuhakikisha kazi zinazotekelezwa zinalingana na thamani ya fedha iliyotumika," alisema.


Alisema Tamisemi imekuwa ikiratibu na kusimamia uchukuaji wa hatua stahiki za kinidhamu na kisheria kwa watumishi, wakandarasi, wahandisi washauri na wazabuni wengine ambao wamekuwa wakibainishwa kwenye taarifa za ukaguzi kujihusisha na vitendo vya ubadhirifu wa fedha za umma.

Bashungwa alisema hadi Februari, mwaka huu Tamisemi imepokea na kuchambua taarifa za ukaguzi maalumu uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwenye halmashauri 64.

"Ofisi za wakuu wa mikoa zimeelekezwa kusimamia uchukuaji wa hatua stahiki za kinidhamu kwa watumishi zaidi ya 1,000 waliotajwa kuhusika na kasoro mbalimbali zilizobainishwa kwenye taarifa hizo," alisema.


Bashungwa alisema Tamisemi imewasiliana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili izifanyie kazi taarifa hizo kwenye maeneo yanayohusu ubadhirifu wa fedha na mali za halmashauri.

Alisema pia Tamisemi inakamilisha uchambuzi wa wakandarasi na wahandisi washauri wote waliotajwa kwenye taarifa za ukaguzi ili wafikishwe kwenye Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) kwa hatua stahiki kutokana na ukiukaji wa maadili ya taaluma zao.

HABARI HIZI ZA UDAKU ZINAPATIKANA KATIKA APP YA UDAKU SPECIAL, IDOWNLOAD>> HAPA BURE 

0 Blogger:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger