Novemba 27, 2020, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alitangaza uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho kuwavua nafasi zote za uongozi wale wote waliokula kiapo kuwa wabunge wa viti maalumu kwa jina la chama hicho. Haitoshi, Mbowe alisema Kamati Kuu Chadema iliwavua uanachama wote 19.
Desemba mosi, 2020, wabunge hao wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee, walifanya mkutano na waandishi wa habari na kueleza dhamira yao ya kukata rufaa Baraza Kuu la Chadema, wakasisitiza “sisi bado ni Chadema”.
Mwaka mmoja na miezi mitano imeshapita tangu tamko hilo la wabunge 19 waliovuliwa uanachama. Sasa kikao cha Baraza Kuu la Chadema kinafanyika keshokutwa.
Mengi yamepita. Je, hasira za awali za waliowafukuza wenzao zipo palepale? Upande wa waliofukuzwa, kuna majuto au bado wanaona hawana kosa?
Kipindi hicho alikuwepo Rais John Magufuli, sasa usukani wa nchi umeshikiliwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Machi 17, 2021, Taifa lilitangaziwa kifo cha Magufuli. Kipindi hicho, Mbowe alikuwa nje ya nchi.
Mbowe aliporejea alianzisha harakati za kudai Katiba Mpya. Katikati ya madai yake, akawekwa mahabusu, akafunguliwa kesi ya ugaidi. Akakaa mahabusu miezi minane.
Swali la kwamba kwa nini Baraza Kuu lilichelewa kuitishwa, ili rufaa ya Mdee na wenzake 18, isikilizwe, linaweza kujibiwa na mazingira ya uongozi wa Chadema.
Kwamba baada ya uamuzi wa Kamati Kuu kuwavua uanachama Halima na wenzake, Mbowe aliondoka nchini. Alirejea baada ya kifo cha Magufuli.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania Bara, Tundu Lissu, baada ya Uchaguzi Mkuu 2020, alikimbia nchi na kwenda uhamishoni Brussels, Ubelgiji. Lissu alikuwa mgombea urais wa Chadema.
Utaona uongozi wa juu wa chama haukuwepo. Nani angeongoza kikao cha Baraza Kuu na kusikiliza rufaa za wanachama hao? Kisha, Mbowe aliporejea nchini, hakuchukua muda mrefu, akawekwa mahabusu na kesi ya ugaidi. Je, chama kingejielekeza kuwasikiliza Mdee na wenzake, wakati Mwenyekiti wao yupo mahabusu?
Keshokutwa, Baraza Kuu litaketi. Bila shaka wahusika watasikilizwa. Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alishatoa taarifa kuwa waliokata rufaa ni wawili tu.
Kwa maana hiyo, kiuhalali, wabunge 17 ambao shauri lao ni mjadala wa nchi tangu Novemba 2020, hawana uhalali wa kusikilizwa?
Je, wabunge hao 17 walisusa kwa sababu waliona hawatatendewa haki? Walijenga kiburi kuwa chama kisingewafanya chochote?
Aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai aliapa kuwalinda kwa vyovyote. Je, wabunge ambao hawakuandika barua kukata rufaa, walikuwa na imani kuwa mbele ya Ndugai hakuna ambaye angewafanya chochote? Ndugai ni mbunge wa benchi la nyuma hivi sasa. Anayeongoza Bunge ni Dk Tulia Ackson. Je, mazingira ni yaleyale?
Spika Tulia alipoulizwa kuhusu uhalali wa wabunge hao, jibu lake lilikuwa wapo bungeni kihalali kwa sababu walikata rufaa kwenye chama chao na hawajasikilizwa.
Je, kama Baraza Kuu la Chadema litakazia uamuzi wa Kamati Kuu kuwa wabunge hao 19 si wanachama, Spika Tulia ataheshimu uamuzi huo? Kwa kuwa Mnyika alishasema waliokata rufaa ni wawili. Je, kabla ya hata hukumu ya Baraza Kuu, Spika Tulia anaweza kuridhia kuwaondoa bungeni wabunge 17, wakati rufaa za wengine wawili zikisubiriwa?
Ipi faida na harasa?
Swali la msingi zaidi ni faida ya kila upande. Kuna manufaa gani Chadema watapa kwa kukazia uamuzi wa kuwafukuza uanachama wabunge hao?
Na je, hasara ni ipi kama wabunge hao wataendelea kuwa ndani ya Bunge? Kinachoangaliwa ni heshima ya chama tu au kuna lingine?
Maandalizi ya kikao
Mmoja wa wajumbe wa Baraza Kuu alisema wameanza kuwasili Dar es Salaam kwa ajili ya kikao hicho kitakachofanyika ukumbi wa Mlimani City.
Alisema kwa kawaida kikao hicho kinakuwa na wajumbe kati ya 500 hadi 600, lakini idadi hiyo inaweza ikapungua kwa sababu mbalimbali ikiwemo baadhi ya wanachama kutokuwa na sifa. Wiki iliyopita, Mnyika aliliambia Mwananchi kuwa maandalizi ya kikao hicho yanakwenda vizuri huku, akisema miongoni mwa ajenda ni kusikiliza rufaa za wabunge wa viti maalumu 19 wakiongozwa na Mdee.
By Luqman Maloto
0 Comments