Heka Heka Angani Baada ya Ingine Moja ya Air Tanzania Kuwaka Moto Ukielekea Mbeya

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA



Hekaheka ndege ya ATCL ikiwaka moto ikielekea Mbeya na abiria 122
Abiria 122 wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), wamenusurika kifo wakiwa safarini baada ya ndege kupata hitilafu.

Ilikuwa Jumamosi Februari 24, 2024, ndege ya ATCL Airbus A220-300 iliyoruka kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya iliponusurika kuteketea ikiwa angani baada ya moja ya injini kuwaka moto.

ATCL imesema tukio hilo limetokea dakika 25 baada ya ndege kuruka.

Awali, ndege hiyo ilipaswa kuanza safari saa 10.00 jioni, kabla ya kusogezwa mbele kwa takribani saa mbili kwa kilichoelezwa kuwa ilikuwa ikisubiriwa kutua Moroni, nchini Comoro.

Abiria aliyekuwa ndani ya ndege hiyo aliyeomba jina lake lisitajwe, amesema baada ya kuruka umbali wa futi anazokadiria kuwa 12,000 walianza kuhisi harufu ya kitu kinachoungua moto.

Baadaye amesema moshi ulianza kuingia ndani ya ndege. Wahudumu walitoa tangazo kuwa kuna tatizo na marubani wanafanya jitihada kuhakikisha usalama unakuwapo.

Ameeleza wahudumu waliwasaidia abiria kuvaa vifaa maalumu vya kuvutia hewa, wakiwasisitiza kuwa na watulivu.

Hata hivyo, amesema hali ndani ya chombo hicho cha usafiri wa anga ilikuwa ya taharuki, abiria kila mmoja akiomba na kusali kwa imani yake.

Amesema baada ya muda kadhaa, moto ulizima na harufu ya moshi ndani ya ndege ikapungua.

“Baada ya jitihada kubwa za marubani iliyochukua saa kadhaa angani (nadhani ya kupeleka ndege juu zaidi pasipo na hewa ya oksijeni), moto ulizimika, ndege ikarejea na kutua salama uwanja wa JNIA saa 3.00 usiku,” amesema alipozungumza na Mwananchi.

Abiria huyo amesema kutokana na hofu ya kifo na taharuki, wengi waliahirisha safari na kurejea majumbani, baadhi wakisalia na kuanza upya safari ya kwenda Mbeya kwa ndege ileile saa 6.00 usiku huohuo.

Shuhuda mwingine ndani ya ndege hiyo, amesema ratiba ya awali kwa mujibu wa tiketi walizokuwa wamekata ndege ilitakiwa kuanza safari saa 10.45 jioni, lakini walipewa taarifa kuombwa radhi na muda ulisogezwa mbele na kuanza safari saa 11.45 jioni.

Amesimulia kabla ya kupitia taharuki hiyo, ndege ilianza kupata mtikisiko mkali.

"Ghafla walianza kutangaza, tunapita kwenye hali mbaya ina mawingu mengi na tusiwe na wasiwasi, kweli tulipita ile hali baada ya muda moshi ulianza kuingia ndani ya ndege," amesimulia.

Amesema muda mchache baada ya kupaa, harufu ya kitu kiuunguacho ilianza, watu wakahamaki kuulizana ni jambo gani bila majibu ya moja kwa moja. Baadaye moshi ulianza kuingia ndani.

"Watu walianza kukohoa na moshi ukawa unazidi, ghafla tukaona wafanyakazi wanaanza kuhangaika na vifaa vya kuzimia moto na wengine wanakimbia kuanzia mwanzo hadi mwisho wa ndege na kuanza kutangaza hali ya hatari na taa za kuonyesha kuna hatari zilianza kuwaka na kuzima," amesimulia.

Amesema moto ulikuwa unatokea upande wa bawa la kulia na hali ilikuwa mbaya. Ameeleza walikuwa anga la mbali, hivyo walikuwa wanaona kama bahari.

Abiria huyo ameeleza wakati watu wanaendelea na taharuki walitangaziwa hali ya hatari wakielezwa hawana namna nyingine, isipokuwa rubani anahangaika kupata mawasiliano wajue sehemu ya kwenda kutua.

Amesema kila mmoja alikuwa anasali kwa imani yake na waliokuwa na tatizo la presha ilipanda kutokana na kile kilichokuwa kinaendelea.

"Ndani ya ndege kuna waliokuwa wanazimia na wengine kumwagiwa maji kama dakika kadhaa, hali ya moshi ikaanza kupotea lakini nilishindwa kujua nini kilitokea hadi ule moto kuzima," amesimulia.

Wakiwa bado wanahangaika angani, amesema muda wote taa ya hatari ilikuwa inazima na kuwaka, huku vilio vya abiria na ibada zikiendelea wakijua kilichobakia ni muda wa kufa tu.

"Ghafla tukiwa huko angani tulitangaziwa rubani amepata mawasiliano sehemu salama ya kutua ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam hivyo tunarudi," amesema.

Amesimulia ndege ikipitia changamoto hiyo, walielezwa na mmoja wa wafanyakazi walikuwa wameshafika katika anga la Mkoa wa Iringa.

"Ile kurudi Dar es Salaam nilikuwa nahisi kama nimepotea angani kwa sababu tulichukua muda mrefu Dar es Salaam, tulipanda ndege saa 11.45 jioni na tulitumia kama saa moja, lakini Dar es Salaam tulikuja kutua saa tatu usiku," anasimulia.

“Mpaka tunatua Uwanja wa Ndege wa JNIA hakuna aliyekuwa anaamini na wengi walighairi safari baada ya kuambiwa wasubiri kwa muda waanze safari kwa ndege ileile waliyopata nayo changamoto wakiwa angani,” ameeleza.

"Tulichokifanya tuliomba mabegi yetu kwa sababu walituambia hata nauli zetu hawawezi kuturudishia na kwamba kilichotokea ni hitilafu ya kawaida baada ya kauli ile ya kukatisha tamaa wenye kuondoka tulifanya hivyo kuanzia saa sita usiku," amesimulia.

Wasiwasi mkubwa

"Abiria walikuwa wanalia na kusalia, lakini wahudumu walikuwa wanakimbia kutoka mwanzo hadi mwisho wa ndege, ni kipindi hicho mimi nilikuwa namwagiwa maji naambiwa nitulie rubani anapambana," amesimulia abiria mwingine.

Amesimulia walikuwa wanachungulia kifo, walikuwa kwenye hali mbaya ya kilio kila kona, wanaume na wanawake.

Ameeleza abiria wengine baada ya kunusurika waliomba kurudishiwa nauli, lakini ombi hilo lilikataliwa.

"Tulikuwa tunaomba turudishiwe nauli zetu kwa sababu tulikosa imani na ndege," amesema.

Anasema baada ya tukio hilo alitarajia ATCL itoe taarifa, kuwaomba radhi na kueleza kilichotokea kilikuwa nini.

"Inawezekana kutokana na hali tuliyopitia wengine tumepata magonjwa moja kwa moja, ingawa hatujui kwa sababu hatujakwenda kupima," amesema.

Kauli ya ATCL

Akizungumza na Mwananchi Digital, Ofisa Uhusiano wa ATCL, Sarah Reuben amekiri Jumamosi ya Februari 24, 2024, ndege ya ATCL aina ya Airbus A220 yenye usajili namba 5H-TCH iliyokuwa ikiruka kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya ilipata hitilafu kwenye injini moja.

Tofauti na inavyoelezwa na abiria, Reuben anasema tatizo hilo lilisababisha moshi ndani ya ndege kwa takriban dakika zisizozidi tano.

Amesema marubani walidhibiti tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kuzima injini yenye hitilafu kama mwongozo unavyoelekeza.

“Rubani alirejesha ndege hiyo Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Dar es Salaam) ikiwa ndiyo kiwanja kilichokuwa karibu chenye uwezo wa ndege ya A220 kutua.

“Wahudumu wa ndege waliendelea kufanya kazi yao kwa weledi mkubwa, ikiwemo kutoa taarifa sahihi kwa abiria kuwa changamoto iliyojitokeza inadhibitika hivyo kuwaondoa hofu,” amesema Reuben.

Hata hivyo, amesema tofauti na inavyoelezwa katika tukio hilo hakuna abiria aliyeonyesha uhitaji wa vifaa saidizi vya upumuaji au kupoteza fahamu.

“Tukio zima lilichukua takriban dakika 60 tangu ndege kupaa angani hadi kurejea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Hata baada ya kurejea Dar es Salaam hakukuwa na abiria yeyote aliyeonyesha changamoto ya kiafya au kuhitaji msaada wowote wa kimatibabu,” ameeleza Reuben.

Kuhusu abiria na safari yao, amesema 104 kati ya 122 waliendelea na safari, 18 wakiomba kubadilisha tarehe za safari, jambo ambalo ATCL ilifanya bila kuwatoza gharama za ziada.

----

Love Story ya NJIA PANDA,Ni Kali mnoo Jamani.

Kusikiliza au kusoma mwendelezo wake Tembelea www.makapedia.com kisha bofya palipoandikwa NJIA PANDA kila siku saa moja kamili jioni BURE au bofya HAPA

Pia Bofya HAPA kujiunga na what's app channel yetu,tukukumbushe kila siku.


-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad