Uteuzi wa Makonda utakavyopisha mabadiliko ya msingi CCM

Nafasi za Ajira Zilizotangazwa Leo Bonyeza Hapa
Uteuzi wa Makonda utakavyopisha mabadiliko ya msingi CCM


Kuna tafsiri anuwai kuhusu mabadiliko ambayo Rais Samia Suluhu Hassan ameyafanya kwenye Baraza la Mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu na naibu makatibu wakuu wa wizara. Majina mawili ni rahisi kuyajengea muktadha unaoeleweka--- Joyce Ndalichako na Deogratius Ndejembi.


Taarifa ya Ikulu ya Machi 31, 2024, iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus, imetaja majina 21 katika uteuzi, uhamisho na utenguzi. Hata hivyo, jina la Paul Makonda ndiyo mada kuu.


Tanzania ni Jamhuri inayoendeshwa katika mfumo wa nusu-urais (semi-presidential republic), ambayo huchukua njia mbili, premier-presidential ambayo Baraza la Mawaziri huwajibika kwa Bunge pekee na president-parliamentary ambayo Baraza la Mawaziri huwajibika kwa Rais kama mkuu wa Serikali, vilevile Bunge.


Tanzania ni semi-presidential, tawi la president-parliamentary. Halafu, Katiba imempa Rais mamlaka ya moja kwa moja ya kufanya atakavyo kwenye Baraza la Mawaziri, wakati Bunge limewekewa mzunguko, ili kuliwajibisha Baraza la Mawaziri.


Kupitia msingi huo uliowekwa kikatiba, Rais hahojiwi anapofanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri. Hata hivyo, haizuiwi kutafsiri hatua anazochukua. Rais anapomwondoa waziri kwenye Baraza la Mawaziri, ni kielelezo dhahiri kwamba hakuridhishwa na utendaji wake.


Kwa mantiki hiyo, Ndalichako ambaye uteuzi wake wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, umetenguliwa ni kipimo kuwa utendaji kazi wake haukumpa alichohitaji, hivyo amemweka kando kutafuta matokeo anayoyataka.


Mambo mawili, tafsiri yake inaweza kukaribia kilichomo ndani ya Rais Samia, nyuma ya utenguzi wa Ndalichako. Mosi, utendaji kazi usioridhisha. Pili, umri. Mei 21, 2024 (siku 50 zijazo), Ndalichako atatimiza umri wa miaka 60.


Jina la wizara ni Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu. Mtu mwafaka anayetakiwa kuiongoza ni kijana. Ndejembi, ana umri wa miaka 40. Julai 12, 2024, atatimiza umri wa miaka 41. Bila shaka, kiumri ni mtu mwafaka kuhudumia wizara inayoshughulikia masuala ya vijana.


Hodi hodi CCM


Mjadala mkubwa ni Makonda kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Arusha. Kabla, Makonda alikuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo. Uteuzi wake unaweza kujenga tafsiri mbili; mosi anapisha mabadiliko makubwa CCM. Pili, kutii malalamiko mengi kuwa Makonda alikuwa akikitumia isivyofaa cheo alichokuwanacho CCM.


Mabadiliko CCM; Machi 12, 2024, Rais Samia, ambaye ndiye Mwenyekiti CCM, alimteua aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu CCM, Tanzania Bara, Anamrigi Macha kuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga. Siku 19 baada ya uteuzi huo wa Macha, Rais Samia, amemteua Makonda.


Uteuzi wa Macha na Makonda, umeacha wazi nafasi mbili kwenye Sekretarieti ya CCM. Hapo hapo, Januari 15, 2024, Dk Emmanuel Nchimbi, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu CCM. Kuingia kwa Nchimbi, kama Mwenyekiti wa Sekretarieti CCM, kuondoka kwa Macha na Makonda, wajumbe wa Sekretarieti, inarahisisha kubashiri mabadiliko makubwa yajayo CCM.


Ongeza mabadiliko mengine; Amos Makalla, ameondolewa kutoka mkuu wa mkoa wa Mwanza na imeelezwa kwamba atapangiwa majukumu mengine. Kadhalika, John Mongella, imeelezwa atapewa majukumu mengine, kutoka ukuu wa mkoa wa Arusha, atakapomwachia ofisi Makonda.


Maelezo kuwa Makalla na Mongella watapangiwa majukumu mengine, jumlisha nafasi zilizoachwa wazi Sekretarieti CCM, inajenga ubashiri kuwa kazi mpya ambazo imeelezwa watapewa ni hizo nafasi zilizobaki wazi CCM.


Makalla, amepata kuwa mjumbe wa Sekretarieti CCM, alipokuwa Katibu wa Nec CCM, Uchumi na Fedha (Mweka Hazina), kati ya mwaka 2007 hadi 2011. Vilevile, alifanya kazi na Nchimbi kwa ukaribu, alipokuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), kipindi hicho Nchimbi alikuwa Mwenyekiti UVCCM.


Kuhusu malalamiko dhidi ya Makonda; alipoidhinishwa na Nec CCM kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Makonda alibeba taswira tofauti. Makonda alianza kuwasema hadharani watendaji wa Serikali aliowaona hawawajibiki, akaonekana kuwa mkubwa ndani ya CCM.


Kwa upande wa Serikali, Makonda alitoa maagizo kwa watendaji, mawaziri mpaka Waziri Mkuu, mambo hayo, yalimfanya aonekane aliyevuka mipaka yake. Hapa kila mtu alitafsiri kwa namna yake.


Mwenye mamlaka ya kumpa maagizo ya kiutendaji Waziri Mkuu ni Rais peke yake. Wenye hadhi ya kuwashurutisha mawaziri na wakuu wa mikoa ni Rais na Waziri Mkuu. Hata hivyo, Makonda akitumia mwavuli wa usemaji wa CCM, aliyavaa mamlaka ya kuwasulubisha watendaji serikalini, aliowaona hawaendi na kasi ya Samia.


Makonda pia alilalamikiwa kwa utoaji wa matamko tata. Machi 26, 2024, ikiwa ni siku tano kabla ya hajateuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Arusha, Makonda alisema kuwa kila anachokifanya Rais Samia, ndicho ambacho kilifanywa na mtangulizi wake, Dk John Magufuli.


Makonda, aliyasema hayo akilenga kufikisha ujumbe kwa watu aliowaita ‘wanafiki’, kwamba wana agenda ya kumtenganisha Rais Samia na Magufuli. Alisema, Rais Samia na Magufuli ni kitu kimoja na haiwezekani kutenganishwa.


Inawezekana Makonda aliona ni sahihi kwake kutamka maneno hayo. Hata hivyo, mtazamo wa kiuchambuzi unakosoa maneno hayo kwa hoja kwamba yanaashiria kumfanya Rais Samia kuwa anayeongoza nchi kwa kivuli cha mtangulizi wake, Dk Magufuli.


Imeshapita miaka mitatu tangu Magufuli alipofariki dunia na Rais Samia kula kiapo cha kuongoza dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mambo mengi yametokea ndani ya miaka mitatu. Mengi miongoni mwa yaliyotendeka, hayafanani hata chembe na mtindo wa uongozi alioutumia Magufuli.


Yapo malalamiko mengine kuhusu Makonda ni kuwa alitumia cheo cha Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, kujijenga yeye binafsi badala ya kuimarisha chama na kuisaidia Serikali ambayo inaongozwa na CCM.


Hakosekani atakayesema kuwa mabadiliko ndani ya Sekreatrieti ya CCM, ndivyo Dk Nchimbi anachanga karata zake, ili kukisuka vema chama hicho. Kama mtendaji mkuu wa chama, anahitaji timu itakayoendana na maono yake, hivyo lazima azungumze na mwenyekiti, Rais Samia, ampe watu anaodhani ni sahihi.


Hata hivyo, pamoja na malalamiko hayo wapo watu waliomuona Makonda kama mtu sahihi kwenye nafasi ya uenezi. Katika muda mfupi akiwa CCM, Makonda alichangamsha siasa hasa kwenye ziara zake zilizokusanya mamia ya wananchi wakiwemo makada wa CCM.


Staili yake ya kutatua kero za wananchi papo kwa papo zilianza kuwavutia wananchi wenye changamoto mbalimbali, japo kwa watendaji zilionekana kuwa mwiba. Makonda hakuona soni kuwapigia mawaziri simu akiwa kwenye mkutano wa hadhara na kuwataka kujibu kero za wananchi.


Kwa mtindo huo, kero za wananchi zilipata majibu na utatuzi wa haraka, huku Makonda akitumia kivuli chake cha cama kuisimamia Serikali yake kuwajibika kwa wananchi.


Sasa anapojiandaa kwenda kuongoza Arusha, kumekuwa na maoni tofauti ikiwemo kwamba, amepelekwa huko kimkakati kutokana na unyeti wa siasa za mkoa huo.


Kelele za vilio na furaha zimeanza kusikika kwenye mitandao ya kijamii, baadhi wakisema jembe limepelekwa Arusha, huku wengine wakisema mbabe na mharibifu wa uchaguzi na demokrasia amepelekwa Arusha.


Mabadiliko zaidi


Ukiacha Makonda, Mongella, Ndalichako, Ndejembi na Makalla, mabadiliko mengine ambayo Rais Samia ameyafanya Machi 31, 2024 yalimhusu Kanali Evans Mtambi, ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara kutoka Mkuu wa Wilaya ya Mkinga. Said Mtanda anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kutoka Mara. Zainabu Katimba, anakuwa Naibu Waziri wa Tamisemi, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Ndejembi.


Daniel Sillo, anakuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, akichukua nafasi ya Jumanne Sagini, ambaye anakuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria. Mhandisi Maryprisca Mahundi, anakuwa Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Tehama, akitoka Wizara ya Maji.


Kundo Mathew anakuwa Naibu Waziri wa Maji, kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Tehama. Fakii Lulandala, amekuwa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, kutoka kuwa Katibu Mkuu UVCCM. Gilbert Kalima ni Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, akitoka kuwa Katibu Mkuu Jumuiya ya Wazazi CCM.


Mhandisi Cyprian Luhemeja, amehamishwa kutoka Ofis ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, sasa ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. Mary Maganga, anakuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.


Dk Edwin Mhede, anakuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, akichukua nafasi ya Agnes Meena, ambaye amehamishwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji. Dk Suleiman Serera, anakuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, kabla, alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro.


Serera anachukua nafasi ya Nicholaus Mkapa, ambaye amehamishwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Tehama. Selestine Kakele ameteuliwa kuwa balozi, kutoka kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Tehama. Dk Asha-Rose Migiro, ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Tume ya Mipango

Mwananchi

_________

 Nafasi za Ajira Zilizotangazwa Leo na Makampuni Bonyeza HAPA

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad