Header Ads Widget


Wabunge wawili wathibitishwa kuwa na corona Kenya



Bunge la Kenya limethibitisha kwamba wabunge wawili wameambukizwa virusi vya corona. 

Wakati anahutubia bunge hii leo, Spika Justin Muturi hatimae amethibitisha kwamba wabunge wawili wameambukizwa ugonjwa wa Covid-19 na sasa hivi wanaendelea kupata matibabu. 

Bwana Muturi amesema kuwa mbunge wa kwanza ametolewa hospitalini na kuruhusiwa kwenda nyumbani ambako anajitenga. 

Mbunge wa pili alikuwa anaumwa lakini sasa hivi afya yake imeimarika na anaendelea kupata afueni hospitalini. 

"Taarifa iliyopo kwa ofisi ya spika inaonesha kwamba wabunge wawili wameambukizwa virusi vya corona," Spika Muturi amesema. 

"Hadi kufikia leo, Juni 30, 2020, mbali na uzushi unaosambazwa na vyombo vya habari, taarifa kutoka ofisi ya spika inaonesha kwamba kuna wabunge wawili walioambukizwa virusi vya corona." 

Aidha Muturi amesema kwamba taarifa za matibabu za wahusika pamoja na utambuzi wao ni siri na hilo litachukuliwa kuwa hivyo. 

"Nikiongezea, vyombo vya habari viache kusisitizia sana corona bungeni kwasababu ni watu kama wengine wale duniani," Muturi amesema. 

Hayo yamejiri huku Wizara ya Afya ikitangaza kwamba watu 176 zaidi wamethibitishwa kupata maambukizi ya virusi vya corona hii leo na idadi hiyo ikifikia jumla ya watu 6,366. 

Dr Rashid Aman, Katibu wa Wizara ya Afya, amesema kuwa 100 kati waliothibitishwa ni wanaume huku 76 wakiwa wanawake. 

Aliongeza kuwa katika kipindi cha saa 24, watu wanne wamekufa na kufikisha idadi hiyo kuwa 148. 

Hadi kufikia sasa 2,039 wamethibitishwa kupona baada ya 26 kuruhusiwa kutoka hospitalini ndani ya saa 24 zilizopita, Dkt Aman amesema.

Post a Comment

0 Comments